TAHARIRI: IEBC isipomulikwa mapema tutajuta
Na MHARIRI
KWA sasa imesalia miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu ujao kuandaliwa.
Licha ya kuwepo kwa mambo mengi yanayotuzonga, ipo haja kwa wadau wakuu kuanza kuwazia mustakabali wa tume hii ya uchaguzi ili kuepuka misukosuko ambayo huibuka kila kura inaponukia.
Baada ya uchaguzi wa 2007/2008 uliofuatiwa na vurumai iliyochangia vifo vya watu zaidi ya 1,000, Tume iliyoongozwa na Krigler ilifanya uchunguzi kwa lengo la kutafuta suluhisho kwa tatizo la vita baada ya uchaguzi.
Katika mapendekezo ya ripoti yake, mojawapo ya suala lililojitokeza bayana ni hali kwamba uchaguzi nchini huandaliwa na tume ambayo huwa ndio mwanzo imeingia ofisini.
Tume za uchaguzi nchini Kenya huwa zinafanyiwa mabadiliko katika kipindi cha lala-salama uchaguzi unapokuwa umenukia. Hali hii huathiri utayarifu wa tume na hivyo kuchangia dosari nyingi katika uchaguzi. Hiki hasa ndicho kiini cha kuwepo kwa kesi nyingi za kupinga matokeo ya kura kuanzia ngazi ya udiwani hadi urais.
Matokeo ya kura za urais siku zote huwa kiazi moto. Huwepo mivutano na makabiliano ambayo huishia mahakamani kama ilivyofanyika mwaka wa 2017 na hata matokeo husika kufutiliwa mbali.
Misukosuko ya baada ya uchaguzi huwa na madhara chungu nzima.Katika baadhi ya maeneo yenye jamii hasimu huzuka vita na hivyo watu kuuawa, maeneo mengine hushuhudia uharibifu mkubwa wa mali na kisasi ambacho hudumu katika nyoyo za watu. Haya yote hufanya uchaguzi mkuu nchini Kenya kuwa zoezi la kufa kupona na linaloogofya mno.
Licha ya ufahamu huu, inashangaza kwamba wadau wakuu ambao ni vyama vya kiasiasa bado hawajaanza kuzungumzia marekebisho katika asasi hii muhimu. Kama kawaida, labda wanasubiri hadi kipindi cha lala-salama. Hulka hii bila shaka itaturejesha pale pale pa kulaumiana na kukimbizana kama wanyama wa mwitu punde matokeo yatakapotangazwa na kisha kupingwa na upande pinzani.
Bunge linafaa kuongoza Wakenya pamaoja mashirika mablimbali ya kijamii kuanza mchakato wa kupiga msasa asasi hii kwa nia ya kuepuka tandabelua la vurugu baada ya uchaguzi.
Tume ya IEBC isipofanyiwa marekebisho mapema hii, itaelekeza taifa pabaya kisha tuanze kulaumiana tena. Ni mtu mpumbavu pekee ambaye miaka nenda miaka rudi hurudia kosa lile lile huku akilia kutokana na masaibu ambayo ana uwezo wa kuyasuluhisha.