Sevilla yaipiga Wolves katika robo-fainali ya Europa League
Na CHRIS ADUNGO
MATUMAINI ya Wolves ya kunyanyua ubingwa wa Europa League kwa mara ya kwanza katika historia yalizimwa na Sevilla waliowadengua kwenye robo-fainali ya kipute hicho mnamo Agosti 11, 2020 mjini Duisburg, Ujerumani.
Sevilla ambao ni wapambe wa soka ya Uhispania, waliwabandua Wolves kwa 1-0 na kufuzu kwa nusu-fainali ambayo kwa sasa itawakutanisha na Manchester United mnamo Jumapili ya Agosti 16, 2020 mjini Dusseldorf, Ujerumani.
Ilikuwa mara ya kwanza katika historia kwa Wolves kupimana ubabe na Sevilla ya Uhispania katika soka ya bara Ulaya.
Chini ya kocha Nuno Espirito, Wolves walipata fursa nzuri zaidi ya kuzamisha chombo cha Sevilla kunako dakika ya 13 ila fowadi Raul Jimenez akapoteza penalti.
Bao la Sevilla lilipachikwa wavuni na Lucas Ocampos mwishoni mwa kipindi cha pili. Goli hilo lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na kiungo Ever Banega.
Wolves kwa sasa hawatakuwa sehemu ya vikosi vya Uingereza vitakavyoshiriki soka ya bara Ulaya msimu ujao baada ya kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu katika nafasi ya saba.
Sevilla ambao ni mabingwa mara tano wa Europa League kwa sasa hawajashindwa katika jumla ya mechi 19 zilizopita katika mapambano yote. Iwapo watawapiku Man-United katika nusu-fainali, basi watakutana ama na Inter Milan ya Italia au Shakhtar Donetsk ya Ukraine kwenye fainali.
Kubanduliwa kwa Wolves ni pigo kubwa kwa kocha Espirito ambaye yuko katika hatari ya kuagana sasa na wanasoka matata waliowatambisha katika kampeni za msimu huu. Kati ya masogora hao ni Jinemez na Adama Traore.
Kampeni za Wolves katika Europa League zilianza Julai 25, 2019 kwa kuwabandua Crusaders kwenye raundi ya kwanza ya mchujo mbele ya mashabiki 29,708 uwanjani Molineux. Ilikuwa mara yao ya kwanza kurejea katika soka ya bara Ulaya baada ya miaka 39.
Sevilla wametinga sasa hatua ya nusu-fainali ya Europa League mara saba. Ni Inter Milan pekee ambao wamefuzu mara nane ndio wanaowazidi.
Wolves walifuzu kwa robo-fainali baada ya kubandua Olympiakos ya Ugiriki kwa mabao 2-1 kwenye hatua ya 16-bora. Kwa upande wao, Sevilla waliwadengua AS Roma kutoka Italia kwenye hatua ya 16-bora kwa jumla ya mabao 2-0.
Miamba hao wa Uhispania ndio wanaojivunia rekodi ya kunyanyua ufalme wa Europa League mara nyingi zaidi na wametawazwa mabingwa katika misimu yote mitatu ambayo imewashuhudia wakitinga hatua ya robo-fainali.
Chini ya mkufunzi Julen Lopetegui, Sevilla wameibuka na ushindi katika mechi sita kati ya saba zilizopita na kichapo cha 1-0 walichopokeza Valencia katika pambano la mwisho la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kiliwakweza hadi ndani ya mduara wa nne-bora jedwalini.