Habari Mseto

Wauzaji mitumba walalamikia agizo

August 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

VALENTINE OBARA na PHYLLIS MUSASIA

WAFANYABIASHARA wa mitumba waliandamana katika miji tofauti Jumatano kutaka kushinikiza serikali iwaruhusu kuagiza bidhaa kutoka nchi za kigeni.

Katika Kaunti ya Nairobi, maandamano yalifanywa katika soko la Gikomba.

Waliohojiwa walisema serikali haijafafanua kuhusu hatima yao na wanahitaji kuambiwa ni lini watakubaliwa kuleta bidhaa ili wajipange kimaisha.

“Wengi wetu tuna madeni ya kulipa kwa stoo zetu kando na mahitaji ya nyumbani. Tunataka kuambiwa iwapo marufuku ya kuleta mitumba itaondolewa, hilo litafanyika lini,” akasema mmoja wa wafanyabiashara.

Katika Kaunti ya Nakuru, walikabiliana na maafisa wa polisi wakati wa maandamano ya kushinikiza serikali iwaondolee vikwazo vya kuingiza mizigo nchini.

Wakati wa maandamano hayo yaliyohushisha mamia ya wafanyabiashara, maafisa wa polisi waliwatawanya kwa vitoa machozi wakidai kuwa walikiuka kanuni zilizowekwa na wizara ya afya ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Kupitia msemaji wao Bw Peter Njoroge, walisema wengi wao wamepoteza ajira katika sekta mbalimbali baada ya viwanda, mikahawa, sehemu za burudani na sekta ya utalii kukosa wateja.

“Tunaomba serikali iruhusu shehena ya nguo kuingia humu nchini ili wafanyibiashara waweze kurejelea hali yao ya kawaida,” akasema.

Mnamo Jumatatu, Waziri wa Biashara, Bi Betty Maina alisema kungali kuna vikwazo kuhusu uagizaji wa bidhaa nyingi kutoka nchi za kigeni.

Vile vile, Bi Maina alisema wengi wao wamepuuza kanuni hizo na kujiweka katika hali hatari jambo ambalo linasababisha serikali kuendelea kuzuia uagizaji wa mizigo ya mitumba.

“Wizara ya afya inapaswa kutoa mwelekeo jinsi ambavyo uagizaji wa migizo hii inapaswa kufanywa na pia kutoa ushauri kuhusiana na hathari zake,” akasema Bi Maina.

Hata hivyo, alihakikishia wafanyabiashara hao kwamba malalamishi yao yatatatuliwa karibuni.

“Kumekuwa na majadiliano mengi na tunazingatia maoni yaliyotolewa kwetu kutoka kwa wafanyabiashara wa mitumba kuhusu jinsi hatari ya maambukizi inaweza kudhibitiwa wakikubaliwa kuendelea kuagiza. Tutajibu mapendekezo yao,” akasema Bi Maina alipohojiwa katika runinga.

Sekta ya mitumba huajiri maelfu ya watu kitaifa.

Kumekuwa na majaribio katika miaka iliyopita kupiga marufuku nguo za mitumba nchini na Afrika Mashariki kwa jumla, lakini juhudi hizo hazijafua dafu.

Wakati janga la corona lilipoingia Kenya, serikali ilianza kuwazia ufufuzi wa viwanda vya nguo ambao ni kigezo cha kupiga marufuku nguo za mitumba.