Kilio cha hospitali za maeneo ya mashambani kwa NHIF
Na CHARLES WASONGA
HOSPITALI za wamiliki binafsi zinazohudumu maeneo ya mashambani zinaitaka Hazina Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) ilipe malimbikizo ya Sh5.6 bilioni zinazoidai kufikia sasa.
Mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa hospitali hizo (RUPHA) Brian Lishenga amesema Alhamisi kucheleweshwa kwa malipo hayo kumewasababishia changamoto za kifedha na kuwalazimu kuwafuta kazi maelfu ya wahudumu wa afya.
Kulingana naye, hospitali hizo pia zimeshindwa kulipa kampuni ambayo huziuzia dawa na vifaa vinginevyo vya afya wakati huu wa janga la Covid-19.
“Tunaomba pesa hizo zilipwe kwa sababu hospitali zote ambazo hutoa huduma za afya maeneo ya mashinani kote nchini sasa zimelazimika kuwaachisha kazo kati ya wafanyakazi 5,000 na 7,000 baada ya NHIF kuchelewesha malipo. Haya ni malipo ya huduma za afya ambazo hospitali zetu zimekuwa zikitoa kwa wanachama wa NHIF,” Dkt Lishenga akawaambia wanahabari jijini Nairobi.
Ameeleza kuwa yeye binafsi amelazimika kuwapiga kalamu kazi wafanyakazi 24 kati ya 53 wanaohudumu katika hospitali yake iliyoko mjini Kitengela.
Naye naibu mwenyekiti wa chama hicho Joseph Kariuki ameelekeza kidole cha lawama kwa mfumo mpya wa teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) ambao umekuwa ukichelewesha utayarishaji wa malipo kwa hospitali zinazotoa hudumu kwa wanachama wa NHIF.
“Japo teknolojia hii ni bora kwa sababu inapunguza ufisadi, tumevunjwa moyo kwamba shida ya kucheleweshwa kwa malipo imejiri tangu matumizi ya ICT ambapo sasa utayarishaji wa malipo umegeuka kuwa chanzo kucheleweshwa kwa malipo hayo hasa wakati huu wa janga la Covid-19,” akasema.
Hospitali hizo za wamiliki binafsi pia zinataka Serikali ya Kitaifa izipe mkopo wa gharama ya chini wakati huu wa janga la corona jinsi ilivyo Sh7 bilioni kwa shule za binafsi.
“Tunaombe tupewe msaada wa vifaa vya kujikinga (PPE) na mahitaji mengine ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona. Hii ni kwa sababu hospitali zetu ndizo zitawahudumia waathiriwa wengi hasa mwezi wa Septemba unaokadiriwa kushuhudia ongezeko la visa vya maambukizi,” Dkt Kariuki akasema.