SRC yapinga pensheni ya wabunge
Na CHARLES WASONGA
TUME ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu ya Watumishi wa Umma (SRC) sasa inataka Rais Uhuru Kenyatta kutotia saini mswada unaopendekeza kuongeza pensheni ya wabunge waliostaafu kati ya 1984 na 2001 hadi Sh100,000 kwa mwezi.
Mwenyekiti wa tume hiyo Lyn Mengich amesema Alhamisi hatua hiyo inakiuka Katiba kwani wabunge hawana mamlaka ya kupendekeza nyongeza ya pensheni ya wenzao waliohudumu zamani kwani huo ni wajibu wa SRC.
Alieleza kuwa sehemu ya 11 ya sheria ya SRC inaitwika wajibu wa kuwasilisha mapendekezo kwa serikali kuhusiana na nyongeza ya pensheni zinazopasa kulipwa watumisha wa umma wa sasa na wale wa zamani, wakiwemo wabunge.
“Kwa hivyo, mswada huo unakwenda kinyume cha kipengele cha 230 (4) (a) cha Katiba kwa sababu ni wajibu wa SRC kupendekeza pensheni ambayo ni manufaa ya wafanyakazi wa zamani. Mapendekezo yoyote ya kuongeza pesheni ya wabunge wa sasa na wale wa zamani sharti yawasilishwe kwa SRC na kukiwa na sababu tosha,” Bi Mengich akasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.
Mswada huo ambao ulidhaminiwa na kiongozi wa wachache bungeni John Mbadi, ulipitishwa na wabunge mnamo Jumatano wiki jana.
Endapo Rais Kenyatta atautia sahihi, jumla ya wabunge 290 waliostaafu kati ya 1984 na 2001 wataanza – kila mmoja – kupokea Sh100,000 kila mwezi kutoka Sh7,000 wanazopokea sasa.
Malipo hayo yataanza kutekelezwa mnamo Julai 1, 2010, ikiwa ni mwongo mmoja uliopita, kulingana na mswada huo, kuashiria kuwa kila mmoja wa wabunge hao wa zamani atapokea malimbikizo ya kiasi cha Sh13 milioni.
Mbadi
Akitetea malipo hayo, Bw Mbadi, alisema mswada wake una nia njema ya kuwakimu wabunge hao ambao alisema baadhi yao kupokea malipo duni ya kati Sh2,000 na Sh6,000 kila mwezi, pesa ambazo haziwezi kukimu mahitaji yao ya kimsingi.
“Pensheni ya Sh100,000 anayopendekezwa kwenye mswada huu ni hela zinazolenga kuwakimu wazee hawa ambao walihudumu katika bunge na wanahitaji fedha za kugharimia chakula na dawa. Inasikitisha kuwa baadhi yao wamekuwa wakifa kutokana na magonjwa mbalimbali, hivyo ni wajibu wetu kujali masilahi yao,” mbunge huyo wa Suba Kusini akaeleza.
Hata hivyo, SRC inasema mswada huo utaongeza mzigo kwa walipa ushuru ambao tayari waanaathirika na janga la Covid-19 kando na kuchochea watumishi wengine wa umma kuitisha nyongeza ya pensheni.
“Hali kama hii itafanya malipo ya pensheni kuwa mzigo mkubwa kwa serikali kuweza kugharimia kutokana na mfuko wa umma. Hii ni kwa sababu nyongeza hii inaweza kupandisha bili ya malipo ya pensheni kutoka Sh27.9 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020 hadi Sh100 bilioni katika mwaka huu wa 2020/2021,” akasema Bi Mengich.