Habari Mseto

Wauzaji bidhaa za wanafunzi walalama Mombasa

August 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MISHI GONGO

WAUZAJI bidhaa za shule katika mji wa Mombasa wanalalamikia hatua ya kufungwa kwa shule hadi mwaka 2021 kuwa ni pigo kubwa kwa biashara zao.

Walisema hali zao za kifedha zinaendelea kuzorota tangu kufungwa kwa shule zote nchini Machi 15 kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19.

Walisema wanahofia kuzama katika dimbwi la uchochole kwani wanalazimika kutumia akiba kulipa ada mbalimbali zikiwemo kodi ya duka na ada za leseni licha ya biashara zao kuwa haziwaingizii kipato chochote.

Aidha walisema baadhi yao wameanza kufunga biashara kwa kushindwa na gharama za kuendesha biashara hizo.

Waliozungumza na Taifa Leo wamesema kufungwa kwa shule kumeathiri pakubwa biashara zao.

Muuzaji viatu na vitabu Bw Brian Osuna amesema tangu kufungwa kwa shule maisha yamekuwa magumu kwake.

“Biashara hii ndiyo iliyonipatia riziki yangu ya kila siku, lakini kwa sasa nashindwa kumudu baadhi ya mahitaji yangu muhimu,” akasema Bw Osuna.

Amesema anahofia kushindwa kumudu kodi ya duka anapohudumu iwapo shule hazitafunguliwa karibuni.

“Nalipa kodi ya duka na kaunti lakini hakuna biashara wakati huu hivyo nalazimika kutumia akiba zangu. Wazazi hununulia watoto wao viatu, sare za shule na vitabu mwanzo mwa mwaka au kila muhula mpya, lakini sasa kusogezwa mbele tarehe ya kufunguliwa shule kutatuathiri pakubwa,” akasema.

Kulingana na Waziri wa Elimu Bw George Magoha shule hazitafunguliwa mwezi Septemba kama walivyokuwa wamepanga awali kufuatia kuongezeka kwa idadi ya maambukizi ya ugonjwa huo nchini.

Bw Magoha aliagiza shule zifunguliwa Januari 2021 ikiwa idadi ya visa vya maambukizi itakuwa imeteremka pakubwa akisema kuwa kufunguliwa kwa shule hizo kwa sasa kutahatarisha afya za wanafunzi.

Mwingine Bw Ali Swaleh anayeuza bidhaa mbalimbali za shule yakiwemo mabegi na vitabu, alisema amelazimika kupunguza mahitaji yake ya kifedha kufuatia hali ngumu ya maisha anayopitia.

“Nimetoka kwa nyumba kubwa niliyokuwa nikiisha nikaguria kwa nyumba ndogo ili kupunguza gharama za maisha,” akasema.

Mwingine Bi Zainab Hamid aliiomba serikali kuwaweka katika orodha ya watu watakaopokea msaada wa vyakula na fedha.

“Tulikuwa tunaweza kumudu maisha yetu lakini kwa sasa wengi wetu tunashindwa. Baadhi ya watu wamefunga milango yao kufuatia kuzorota kwa biashara. Hatujui hali ya kawaida itarudi lini hivyo twaomba serikali ituangalie,” akasema.