Habari

Raila amruka nduguye Oburu kwa kupayuka kuhusu 2022

August 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amejitenga na kauli ya ndugu yake Oburu Odinga na Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe kuwa 2022 atasaidiwa kuchaguliwa Rais kwa njia za mkato.

Bw Odinga alisema Alhamisi kauli za wawili hao zilikuwa ni maoni yao watu binafsi na yasiyo na msingi.

Bw Odinga pia alipuuzilia mbali madai yaliyotolewa na Naibu wa Rais William Ruto kuwa kuna kundi lenye ushawishi mkubwa ambalo linapanga kuiba kura katika uchaguzi ujao ili kumzuia kuingia Ikulu.

“Mimi sina wadhifa wowote katika serikali ya Kenya. Kenya inaongozwa na Uhuru na Ruto. Kama kuna kundi la watu wenye ushawishi mkubwa serikalini basi ni rais na naibu wake,” akasema Bw Odinga.

Wiki iliyopita Bw Oburu alidai kuwa Bw Odinga atashinda urais wa 2022 kwa sababu ataungwa mkono na kundi la watu wenye ushawishi mkubwa.

“Raila amekuwa akipoteza uchaguzi wa urais kila mara kwa sababu kuna kitu kimoja ambacho amekosa. Hajawahi kuungwa mkono na kundi ambalo hufanya uamuzi kuhusu nani anakuwa Rais wa Kenya. Lakini wakati huu anaungwa mkono na kundi hilo na hivyo atakuwa Rais 2022,” akasema Bw Oburu.

Bw Murathe naye aliwataka Wakenya kujiandaa kwa ajili ya utawala wa Bw Odinga kuanzia 2022.

Kauli ya Murathe

Bw Murathe ambaye ni mmoja wa wandani wa karibu wa Rais Kenyatta, alisema kuwa Bw Odinga ataongoza kwa muhula mmoja na kisha kuwaachia viongozi vijana.

Wakati huo huo, Bw Odinga ameshikilia kuwa kura ya maamuzi ya kufanyia Katiba marekebisho itafanyika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022 akisema kuna fedha za kutosha kuandaa shughuli hiyo.

“Kura ya maamuzi inahitaji Sh1 bilioni pekee. Uchaguzi huwa ghali nchini kutokana na ufisadi. Tuko tayari kumwonyesha mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati jinsi ya kuandaa kura ya maamuzi kwa kutumia chini ya Sh2 bilioni,” akasema Bw Odinga.

Alisema yeye na Rais Kenyatta wako tayari kupokea ripoti ya mwisho kutoka kwa Jopokazi la Mpango wa Maridhiano (BBI).

“Watu wamekuwa wakieneza porojo kuhusu BBI. Ukweli ni kwamba tuko tayari kupokea ripoti hiyo. BBI haijafa bali tulikuwa tumeenda mapumzikoni,” akasema Bw Odinga.