• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Gor yalemewa na Hull City kwa penalti licha ya Oluoch kupangua tatu

Gor yalemewa na Hull City kwa penalti licha ya Oluoch kupangua tatu

Na GEOFFREY ANENE

KIPA Boniface Oluoch alipangua penalti tatu, lakini kazi yake haikutosha kuinasua Gor Mahia kutoka kwa kichapo cha penalti 4-3 dhidi ya wageni Hull City uwanjani Kasarani, Jumapili.

Dakika 90 zilikamilika 0-0 kabla ya Hull kuonyesha weledi wake wa kupiga penalti ikivuna ushindi kupitia penalti za Jon Toral, Kevin Stewart, Billy Chadwick na Robbie McKenzie.

Gor ilianza upigaji wa penalti vibaya baada nahodha Harun Shakava kugonga mlingoti. Hata hivyo, ilibahatika kusalia 0-0 baada ya Oluoch kudaka penalti ya Jarrod Bowen.

Mrwanda Meddie Kagere aliipa Gor uongozi alipofuma penalti safi kabla ya Tom Powell kuipa Gor hata matumaini zaidi ya kushinda alipopoteza penalti ya pili ya Hull iliyodakwa na Oluoch.

Mrwanda Jacques Tuyisenge aliimarisha uongozi wa Gor hadi 2-0 kabla ya Toral kumwaga Oluoch na kufanya mambo kuwa 2-1.

Wapigaji wa nambari ya nne Wesley Onguso (Gor) na Brandon Fleming (Hull) walipoteza penalti zao kabla ya Gor kupata pigo Cersidy Okeyo alipopoteza penalti yake naye Kevin Stewart akafungia Hull. Samuel Onyango alirejesha matumaini ya Gor, lakini Kevin Omondi akapoteza penalti yake nao Chadwick na McKenzie wakahakikishia wageni hao ushindi.

Gor itajilaumu yenyewe kupoteza mchuano huu hasa baada ya kutawala muda wa kawaida na hata kupata nafasi kadhaa nzuri zilizopotezwa na Ephrem Guikan, Francis Kahata na Tuyisenge.

Vikosi (wachezaji 11 wa kwanza):

Gor Mahia – Boniface Oluoch, Philemon Otieno, Godfrey Walusimbi, Joash Onyango, Ernest Wendo, Francis Kahata, Jacques Tuyisenge, Ephrem Guikan na George ‘Blackberry’ Odhiambo. Kocha – Dylan Kerr (Uingereza).

Hull City – David Marshall, Dan Batty, Stephen Kingsley, Robbie McKenzie, Adam Curry, Kevin Stewart, Evandro, Jarrod Bowen, Will Keane, Jon Toral na Fraizer Campbell. Kocha – Nigel Adkins (Uingereza).

You can share this post!

Kocha mpya wa Stars ataja kikosi cha wachezaji 21

Ngelel na Mukhwana washindwa kutetea mataji Dalian Marathon

adminleo