Lusaka awaita maseneta kwa mara ya tisa kujadili mgao wa fedha
Na CHARLES WASONGA
SENETI itafanya kikao maalum Jumatatu wiki ijayo katika jaribio la mwisho kutanzua mvutano kuhusu mfumo wa ugavi fedha baina ya kaunti baada ya kikao kilichoratibiwa kufanyika Alhamisi kutofanyika.
Kwenye tangazo lilichapishwa katika gazeti rasmi la serikali toleo la Ijumaa, Spika wa bunge hilo, Kenneth Lusaka, alisema kikao hicho kitaanza saa nne asubuhi ambapo suala hilo ndilo litakuwa ajenda ya kipekee itakayoshughulikia siku hiyo.
“Kulingana na kanuni ya seneti nambari 30, shughuli iliyojwa ndiyo itakuwa ajenda ya kipekee katika kikao hicho cha maalum. Baadaye seneti itaahirisha shughuli hadi Jumanne Septemba 8, 2020, kulingana na kalenda ya Seneti,” akasema.
Kikao hicho kitakuwa na cha tisa kuwahi kuandaliwa na maseneta kujadili mfumo huo utakaotumika kugawanya Sh316.5 bilioni zilizotengewa serikali za kaunti katika mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021.
Suala hilo limegawanya maseneta kuwili; wale wanaunga mfumo uliopendekezwa na Kamati ya Fedha ambapo kaunti 29 zitaongezewa fedha huku kaunti 18 zikipunguziwa mgao wa fedha.
Maseneta kutoka Kaunti za Pwani, Kaskazini Mashariki na Ukambani ambazo zitapoteza fedha wamepinga mfumo huo wakisema ni pigo kwa ugatuzi kwani utakwamisha mipango ya maendeleo katika kaunti hizo.
Kikao cha Jumanne wiki jana kiliahirishwa baada ya maseneta kupitisha pendekezo la Seneta wa Meru Mithika Linturi kwamba kaunti zigawanye Sh270 bilioni kwa usawa kisha Sh46.5 bilioni zigawanywe kwa misingi ya mfumo uliopendekezwa na kamati ya fedha.
Kulingana na Bw Linturi pendekezo lake litachangia kupungua kwa kiasi cha fedha ambazo kaunti 18 zitapoteza sawa na zile ambazo kaunti 29 zitaongezewa.
Kwa mfano, badala ya Kaunti ya Mandera kupoteza Sh2 bilioni chini ya mfumo wa kamati ya fedha sasa itapoteza Sh160 milioni pekee chini ya mfumo huu mpya.
Kaunti ya Kiambu nayo itaongeza Sh222 milioni zaidi badala ya Sh1.3 bilioni ilivyopendekezwa na kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kirinyaga Charles Kabiru.
Mnamo Jumanne Spika Lusaka aliahirisha kikao cha Seneti saa tatu za usiku maseneta walipokuwa wakijadili pendekezo la Seneta Maalum Petronilla Were.
Kulingana na Seneta huyo wa ANC akaunti zinapasa kugawanya Sh316.5 bilioni kwa msingi ya mfumo wa sasa na mfumo huo mpya uanze kutumika wakati ambapo Hazina ya Kitaifa itaongeza mgao kwa kaunti hadi Sh348 bilioni.