Willian sasa mali rasmi ya Arsenal
Na CHRIS ADUNGO
ARSENAL wamekamilisha usajili wa aliyekuwa kiungo wa Chelsea, Willian Borges da Silva, 32, kwa mkataba wa miaka mitatu.
Nyota huyo mzawa wa Brazil alibanduka uwanjani Stamford Bridge bila ada yoyote baada ya Chelsea kukataa kurefusha kandarasi yake kwa miaka mitatu aliyoitaka na badala yake kusisitiza kwamba wangempa mkataba wa miezi 24 pekee.
“Ni mwanasoka wa haiba kubwa atakayeleta tofauti kubwa katika safu ya kati ya Arsenal. Anakuja na nguvu mpya itakayoaamsha viwango vya ushindani katika idara ya kati na safu ya mbele,” akasema Arteta.
Willian aliondoka Chelsea mwishoni mwa msimu huu wa 2019-20 baada ya kuwachezea jumla ya mechi 339 zilizomshuhudia akiwashindia jumla ya mataji matano, yakiwemo mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Alisajiliwa na Chelsea kutoka Anzhi Makhachkala ya Urusi mnamo 2013 kwa kima cha Sh4.2 bilioni.
Akiwa Chelsea, aliwahi kutawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka kambini mwa kikosi hicho mara mbili.
“Ni mchezaji aliye na uwezo wa kuwajibishwa katika nafasi nafasi tatu au nne kwenye safu ya kati na mbele. Anajivunia tajriba pana katika soka ya EPL na analeta maarifa na ubunifu ambao tunahitaji sana kwa minajili ya kampeni za muhula ujao,” akaongeza Arteta.
Arsenal walikamilisha kampeni za EPL msimu huu katika nafasi ya nane jedwalini huku Chelsea wakifunga mduara wa nne-bora na kujikatia tiketi ya kunogesha kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.
Hata hivyo, Arsenal waliwapepeta Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo Agosti 1, 2020 uwanjani Wembley, Uingereza. Willian alikosa mechi hiyo iliwapa Arsenal nafasi ya kufuzu kwa soka ya Europa League msimu ujao kwa sababu ya jeraha la mguu.
Willian anamfuata raia mwenzake wa Brazil, beki David Luiz kambini mwa Arsenal baada ya nyota huyo wa zamani wa Paris Saint-Germain (PSG) kusajiliwa na Arsenal mnamo Agosti 2019.
“Namjua Willian vizuri na ninatambua ukubwa wa uwezo alionao uwanjani. Namfahamu kwa sababu nimewahi kufanya kazi pamoja naye katika timu ya taifa ya Brazil. Ana sifa nzuri za uanaspoti na atahitaji muda mfupi sana kuoanisha mchezo wake na wenzake kambini mwa Arsenal,” akasema mkurugenzi wa spoti wa Arsenal, Eduardo Cesar Daud Gaspar.