Makala

UMBEA: Hakuna atakayekushikia fimbo umpende ama usimpende mtu

August 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SIZARINA HAMISI

MAZOEA huleta kukinai na hali hii ipo katika uhusiano, ndoa ama mapenzi.

Kwamba kila afanyalo mwenzio, wewe unahisi kichefuchefu, unatamani akuondokee angalau upate kupumua. Inapofikia hatua hii unaweza ukahisi umemchoka mpenzi wako.

Unaweza kujikuta umeanza kufikiria yule mwenzako uliye naye sio sahihi kwako na hutaki kuendelea naye.

Ukijisikia hivi usishangae ama kujilaumu sana, kwani ni kawaida kwenye uhusiano kujisikia hivi wakati mwingine.

Nitakayozungumza hapa leo hayawahusu sana wanandoa, bali akina dada walio katika uhusiano wa kawaida wa kimapenzi.

Mapenzi ni hisia za ndani, uamuzi wa kuendelea na mtu katika hatua ya uchumba ambayo huambatana na ndoa. Uamuzi huu ni wa mhusika mwenyewe. Hakuna atakayekushikia fimbo ama kukulazimisha umpende ama usimpende mtu fulani.

Mnapokuwa kwenye uhusiano ni kipindi chenu cha kuchunguzana vizuri. Kila mmoja lazima amjue mwenzake sawasawa, hii itamsaidia kila mmoja kufahamu anakwenda kuingia kwenye ndoa na mtu wa aina gani. Lakini aghalabu hutokea unahisi huwezi kuendelea tena na uhusiano na mwenzako na kwamba wakati umewadia wa kuachana.

Huenda umegundua kwamba mwenzako hakufai (kwa sababu zako binafsi) ambazo kwa hakika huwezi kumweleza. Lakini ukitafakari jinsi ya kuachana naye, mwenzako anakuwa amekolea kwa upendo kwako. Inawezekana umejaribu kupima sababu zako na ukagundua hazina uzito ama sio za msingi.

Sababu ambazo huwezi kumwambia mpenzi wako, lakini moyo umekuthibitishia kwamba huyo si chaguo lako na uking’ang’ania kuendelea naye basi furaha katika maisha yako itakuwa ni sawa na kitendawili kigumu mno.

Hali hii ni kawaida na mara nyingi na suluhisho lake sio kuachana na mwenzako kwa jazba, inabidi ufanye tathmini.Ni muhimu ujiulize kwa nini unataka kumwacha mwenzako. Hii ni hatua ya kwanza na muhimu. Kama nilivyosema awali, ni vyema kuuchunguza moyo wako, maana isije ukamwacha kwa sababu ya tamaa zako au umeleweshwa kimapenzi na mwingine, ukashawishika kwa nje, ikiwa hizi ndio sababu zako unajiweka katika hali ya utata na baadaye unaweza kujutia hatua yako.

Sababu kubwa ya kuachana kwenu inatakiwa iwe ile ya kutafuta amani ya moyo wako, maana umeshajichunguza na umegundua kwamba, kulazimisha kuendelea naye, maana yake utaishi maisha yasiyo na amani. Kama ndivyo, wazo hili ni sahihi, lakini kumbuka hutakiwi kumwumiza mwenzako wakati ukitekeleza jambo hili ambalo ni matakwa yako binafsi.

Halafu jiulize iwapo hizi sababu zinazungumzika. Zipo sababu kuu mbili za kutaka kusitisha uhusiano. Ya kwanza nilishaifafanua kwenye kipengele kilichotangulia, lakini ya pili sasa ni kama kweli ana kasoro ambazo unaweza kumweleza moja kwa moja.

Kumbuka njia nitakazokueleza hapa ni za muda mrefu, zinahitaji ufundi na inategemea na namna mwenzako atakavyopokea, hivyo kama unajua mwenzako hajatulia na ushahidi unao, zungumza naye wazi kuliko kumzungusha.

Ukishayatenda hayo yaliyotangulia, punguza naye mawasiliano. Silaha ya kwanza ya mapenzi ni mawasiliano. Kuwasiliana ndipo kunapodumisha penzi ama pia kuliporomosha.

Punguza kumpigia simu au kumwandikia ujumbe mfupi. Akikupigia yeye pokea, akituma ujumbe mfupi unaweza kujibu na wakati mwingine kuacha. Akikuuliza, mwambie una mambo mengi. Hii ni alama ya kwanza itakayomfanya ahisi uhusiano wenu umeanza kuyumba. Muhimu utambue kwamba kuachana na mtu uliyempenda kwa dhati ni mtihani mgumu, unahitaji kuamua na kujitolea kwani bila hivyo utajikuta ukiyumba huku na kule.

Hata hivyo pia ujue hisia ya kumchoka mwenzako ni ya kawaida na wakati mwingine suluhisho sio kuachana naye bali kutathmini tofauti zilizojitokeza na kuzipatia suluhu.

[email protected]