• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
Misikiti yafunguliwa Algeria kwa mara ya kwanza baada ya miezi minne

Misikiti yafunguliwa Algeria kwa mara ya kwanza baada ya miezi minne

Na MASHIRIKA

ALGIERS, Algeria

ALGERIA Jumamosi ilianza kufungua misikiti, mikahawa, fuo za bahari na bustani za kubarizi baada ya kuzifunga kwa miezi mitano kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Serikali ya nchi hiyo ilisema imeanza kulegeza masharti ya kuzuia corona yaliyodumu kwa muda mrefu ulimwenguni. Hata hivyo ilidumisha amri ya kutotoka nje usiku katika nusu ya nchi hiyo.

Raia wote wanatakiwa kuvaa barakoa katika maeneo ya umma. Serikali ilisema iliamua kulegeza kanuni kwa sababu maambukizi yamepungua.

Mnamo Jumamosi watu walimiminika katika fuo za bahari ya Mediterranean jijini Algiers kusherehekea kwa kuogolea msimu huu wa joto. Mikahawa pia uliruhusiwa kufunguliwa na misikiti ambayo inaweza kuingia watu zaidi ya 1000 ili kuhakikisha kuna umbali wa kutosha baina ya watu.

Hata hivyo, wanawake, watoto na watu walio na umri mkubwa hawataruhusiwa kuhudhuria ibada misikitini. Ibada kuu za Ijumaa pia hazitaruhusiwa ili kuepuka umati. Watakaohudhuria ibada lazima wavalie barakoa na kubeba mikeka yao binafsi kutoka nyumbani.

“Kulegezwa kwa masharti haya kutategemea nidhamu ya mtu binafsi kutii kanuni za kujikinga,” alisema waziri wa masuala ya kidini Mohamed Belmahdi, aliyekuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuhudhuria ibada katika msikiti wa Khaled Ibn El Walid mjini Heuraoua ulio mashariki ya Algiers mnamo Jumamosi. Alionya kuwa serikali haitasita kufunga misikiti iwapo raia wa Algeria watakiuka kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona. “ Afya ya raia inatangulia imani,” alisema.

Kufikia Ijumaa, Algeria ilikuwa imeripoti visa 37,000 vya maambukizi ya corona na vifo 1,350 ikiwa ya tatu barani Afrika baada ya Afrika Kusini na Misri.

  • Tags

You can share this post!

Olympique Lyon ya Ufaransa yaendeleza ubabe dhidi ya...

Wahamiaji haramu wanaoingia Italia waongezeka