SIHA NA LISHE: Vyakula hivi ni muhimu kwa wanaougua kisukari
Na MARGARET MAINA
Parachichi
PARACHICHI linajulikana kwa kuwa na mafuta mazuri kwa ajili ya moyo.
Mafuta ya namna hii kama yanayopatikana kwenye tunda la parachichi yanaweza kuweka sawa usawa wa lehemu mwilini, yanaweza yakampunguzia mtu hatari ya kupata magonjwa ya moyo. Sababu hizi zinafanya na hivyo kuwa tunda zuri kwa mtu mwenye kisukari.
Wakati huo huo parachichi moja lina nyuzinyuzi na wanga.
Maharagwe
Maharagwe yana nyuzinyuzi za kutosha. Maharagwe pia yana protini bora kabisa kuliko zote, isiyo na madhara kama ile inayopatikana kwenye nyama na hizi ndizo sababu zinazofanya maharagwe yawe ni chakula kizuri sana kwa mtu mwenye kisukari na mwenye shinikizo la juu la damu pia.
Vile vile kutumia vyakula vyenye nyuzinyuzi zaidi kunakuondolea hatari ya kukumbwa na mshtuko wa moyo.
Maharagwe yana kiasi kidogo cha wanga na kiasi kingi cha protini, magnesium na amino acids.
Samaki
Samaki ni chakula bora kwa mgonjwa wa kisukari. Samaki huwa na Omega 3 ambayo ni nzuri kwa mtu anayetaka kuepuka lehemu na kisukari kwa ujumla.
Omega 3 pia ni nzuri kwa mtu mwenye presha ya kupanda na hupunguza uwezekano wa kutokea tatizo la kupoteza kumbukumbu.
Kitunguu saumu
Kitunguu saumu ni kiungo kizuri kwa chakula na pia ni dawa nzuri sana kwa magonjwa mbalimbali mwilini ikiwemo kisukari.
Hata hivyo, ili kitunguu saumu kiwe kizuri kama tiba, ni vizuri kitumike kibichi; yaani bila kupikwa katika moto.
Tufaha
Kuna msemo wa kizungu unaosema: ‘An apple a day keeps the doctor away’, kumaanisha kula tunda moja la tufaha kwa siku kunaondoa uhitaji wa daktari hasa daktari wa matatizo ya moyo.
Kula tufaha moja tu kwa siku kunaweza kupunguza lehemu mbaya. Kuna aina ya viondoa sumu vilivyomo kwenye tufaha ambavyo huwezi kuvipata sehemu nyingine yoyote na ndivyo vinavyolifanya tunda hili kuwa tunda muhimu zaidi kutumika na mtu mwenye kisukari kila siku.
Karoti
Karoti zina kiasi kingi cha vitamini A, viuavijasumu muhimu ‘beta-carotene’.
Vitamini A ni muhimu sana kukabili matatizo ya macho, kuzuia kansa na ni kinga ya mwili. Hivi ni vitu muhimu sana kwa mtu anayesumbuliwa na kisukari.