Baadhi ya wakazi Mombasa wapinga mpango wa masomo mashinani
Na MISHI GONGO
BAADHI ya wazazi katika Kaunti ya Mombasa wameupinga mpango wa masomo mashinani – community based learning- uliopendekezwa na serikali wakisema mpango huo unahatarisha hali za kiafya za watoto wao.
Walisema kujumuika kwa watoto kutoka nyumba tofauti ili kupokea masomo kutachangia watoto kuambukizana Covid-19 iwapo mmoja kati yao atakuwa ameathirika.
“Katika takwimu za Wizara ya Afya tumeona kuwa watoto hawajasazwa na ugonjwa huu. Tunahofia kupoteza watoto wetu iwapo mikakati muafaka haitafuatwa kuhakikisha usalama wao,” akasema mkazi wa Bombolulu Bw Juma Fadhili.
Kulingana na msimamizi wa Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) Bi Nancy Macharia mpango huo ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaendelea kudurusu licha ya shule kufungwa.
Alisema mpango huo utahusisha wakuu katika sekta ya elimu na maafisa wa afya kuhakikisha unafanikishwa.
Mkurugenzi wa TSC mjini Mombasa Bw Samuel Marigat alisema Jumatano wiki jana walifanya mchakato wa kuwasajili walimu katika kaunti hiyo.
“Tumeanza kwa kuwasajili walimu na sehemu wanazoishi,” akasema.
Alisema kila mwalimu atahudumia kundi la wanafunzi 15.
Kuhusu sehemu watakazo kongamana kwa ili kutekeleza mpango huo,Bw Marigat alisema bado wanajadiliana kuona ni sehemu gani muafaka amabazo walimu watatekeleza shughuli hiyo.
“Walimu watawafundisha watoto mtaani wanako ishi,” akasema.
Aidha alisema bado wanajadiliana kujua iwapo walimu na wanafunzi watapimwa ugonjwa wa COVID 19 kabla kuanza mpango huo au la.
Alisema wanafunzi wataanza kufunzwa wiki ijayo.
Mzazi mwengine Bi Jane Wambui alisema kuwakusanya wanafunzi katika mpango huo kutaleta maambukizi zaidi.
“Watoto hawajui kujikinga, wakati wakucheza hawatakosa kugusana na pia kutumia vitu pamoja hivyo kujiweka katika hatari ya kuambukizwa,” akasema.
Walimu walioongea na Taifa Leo walilalamikia kuwa mpango huo utawapa wakati mgumu kufuatia shule tofauti kutofautiana katika kumaliza silabasi.
“Wanafunzi katika shule tofauti itakuwa ni vigumu kuwafunza kwa pamoja.wanafunzi hawa kwanza wako katika mada tofauti kuna wale wanakaribia kumaliza silabasi wengine wako kati kati na kuna wale wako mwanzoni hivyo ni vigumu kuwaeka pamoja,” akasema mwalimu mmoja aliyekataa kutajwa.
Aliiomba serikali kuja na mipango ambayo itakuwa salama kwa wanafunzi na haitakuwa changamoto kwa walimu.
Kulingana na Waziri wa Elimu Prof George Magoha shule zinapangwa kufunguliwa mwaka 2021 ikiwa mkurupuko wa virusi vya corona nchini utakuwa umepungua.