Habari Mseto

Afisa wa kaunti motoni kuhusu wizi wa hati

August 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

NAIBU wa karani mkuu kaunti ya Bungoma alishtakiwa Ijumaa kwa wizi wa hati za bajeti ya kaunti ya hiyo za mwaka wa 2020-2021.

Francis Simiyu alikanusha mashtaka mawili  dhidi yake mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Kibera Bw Charles Mwaniki Kamau.

Simiyu alishtakiwa siku nne baada ya mwanaharakati Barasa Nyukuri kuachiliwa na Bw Kamau akawasilishe hoja wa kumtimua mamlakani Gavana Wycliffe Wafula Wangamati.

Hoja ya kumbandua mamlakani Bw Wangamati ilikuwa imeorodheshwa kuwasilishwa Jumanne katika bunge la kaunti ya Bungoma.Haikuendelea.

Bw Nyukuri aliachiliwa Jumatatu bila masharti na hakimu asafiri hadi Bungoma kuwasilisha hoja ya kumwonyesha mlango Gavana Wangamati.

Hata hakimu aliamuru polisi wasimtie nguvuni Bw Nyukuri akisafiri usiku wa Jumatatu.

Polisi walikuwa wakitaka Bw Nyukuri azuiliwe kwa siku 15 lakini mahakama ikasema “ombi hilo halina mashiko kisheria na kuitupilia mbali.”

Hakimu alikuwa amefahamishwa na mawakili Suyianka Lempaa na Bryan Khaemba, polisi wanatumiwa vibaya na wanasiasa kukandamiza haki za Bw Nyukuri.

Akimwachilia Bw Nyukuri , hakimu alisema “ sababu za kutiwa nguvuni kwa mwanaharakati huyo zilikuwa za kisiasa.”

Aliposhtakiwa mbele ya Bw Kamau, mshtakiwa alikanusha mashtaka mawili na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

Kiongozi wa mashtaka Bw George Obiri hakupinga ombi hilo la Bw Simiyu la kuachiliwa kwa dhamana.

Hakimu alimwamuru mshtakiwa alipe dhamana ya Sh30,000 pesa tasilimu.

Shtaka la kwanza dhidi ya Simiyu lilisema mnamo Julai 7 katika afisi za bunge la kaunti ya Bungoma aliiba faili ya idara ya teknologia na usimamizi iliyokuwa na makadirio ya matumizi ya pesa katika bajeti ya mwaka wa 2020-2021.

Shtaka la pili lilisema mshtakiwa alipatikana na faili hiyo katika kituo cha mafuta ya petrol kilicho mtaani Langataa Nairobi mnamo Agosti 6 2020 akijua imeibwa au kupatikana kwa njia isiyo halali.