• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
PSG wawapepeta RB Leipzig 3-0 na kufuzu fainali ya Uefa Champions League

PSG wawapepeta RB Leipzig 3-0 na kufuzu fainali ya Uefa Champions League

Na CHRIS ADUNGO

MIAMBA wa soka nchini Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG) waliwapepeta RB Leipzig 3-0 kwenye nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) jijini Lisbon, Ureno mnamo Agosti 18, 2020, na kufuzu kwa fainali ya kipute hicho kwa mara ya kwanza katika historia.

Mabao ya PSG ambao ni miongoni mwa vikosi vinavyofahamika kwa kutumia fedha nyingi zaidi sokoni kwa minajili ya wanasoka wapya wa haiba kubwa, yalifumwa wavuni kupitia kwa Marquinhos, Angel Di Maria na Juan Bernat.

Marquinhos ndiye aliyefungia PSG mabao mengine mawili ya dakika za mwisho kwenye kivumbi cha nusu-fainali kilichowashuhudia wakiwang’oa Atalanta kwenye hatua ya nane-bora.

Ushirikiano mkubwa kati ya Neymar na Di Maria uliwalemaza kabisa Leipzig ambao walisalia kumtegemea pakubwa kipa wao Peter Gulacsi aliyefanya kazi ya ziada kwa kupangua mengi ya makombora aliyoelekezewa na mafowadi wa PSG.

PSG kwa sasa wanatazamia kunogesha fainali itakayowakutanisha na mshindi kati ya Bayern Munich kutoka Ujerumani na Olympique Lyon ya Ufaransa. Nusu-fainali hiyo ya pili itandazwa leo Jumatano ya Agosti 19 jijini Lisbon huku fainali ikiratibiwa kupigwa Jumapili ya Agosti 23, 2020. Bayern ni mabingwa mara tano wa taji la UEFA.

Kabla ya PSG kufunga bao la pili, Leipzig walikuwa wamepoteza nafasi mbili za wazi za kutikisa nyavu za wapinzani wao kupitia kwa Yussuf Poulsen na Dani Olmo.

Katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita, PSG walikabiliwa na nuksi ya kuaga mapema kivumbi cha UEFA ambapo wameondolewa kwenye hatua ya 16-bora. Kabla ya hapo, walikuwa wamebanduliwa kwenye hatua ya robo-fainali katika kipindi cha miaka minne mfululizo.

Matokeo hayo duni yalikuwa kiini cha kutimuliwa kwa waliokuwa wakufunzi wao Laurent Blanc na Unai Emery.

Chini ya kocha Thomas Tuchel ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Borussia Dortmund, PSG wamefuzu kwa fainali ya UEFA kwa mara ya kwanza tangu 1997 ambapo walitawazwa mabingwa wa Cup Winners’ Cup. Wakati huo, Mbappe, 20, hakuwa amezaliwa.

You can share this post!

Washtakiwa kuiba maziwa

Wapinzani wangu wataisoma namba – Ferguson Rotich