Rais IBK wa Mali ajiuzulu baada ya kukamatwa na wanajeshi
Na MASHIRIKA
BAMAKO, Mali
RAIS wa Mali Ibrahim Boubacar Keita amejiuzulu mapema Jumatano baada ya wanajeshi waliozua ghasia kumkamata na kumzuilia katika kambi ya kijeshi iliyoko mjini Kati, kilomita chache kutoka jiji kuu la Bamako.
Keita, Waziri Mkuu Boubou Cisse, mawaziri na maafisa wakuu wa serikali walikamatwa Jumanne na wanajeshi hao.
Kwenye taarifa fupi iliyopeperushwa kwenye runinga kutoka kambi ya kijeshi ya Kati alipozuiliwa, Keita aliyeonekana mchovu alisema hakutaka nchi kukumbwa na umwagikaji wa damu.
“Leo, baadhi ya vikosi vya wanajeshi wameuamua kuingilia kati. Nina chaguo kweli? Kwa sababu sitaki damu imwagike,” Keita alisema.
“Kuanzia sasa, nimeamua kuacha majukumu yangu ya urais,” alisema.
Sasa jeshi limesema litatwaa mamlaka – awamu ya mpito – katika nchi hiyo.
Mataifa ya Afrika Magharibi na Ulaya yamelaani hatua ya jeshi ya kuzua ghasia.
Kanali Jenerali Ismael Wague ambaye kufikia sasa ni naibu kiongozi wa watumishi katika jeshi la wanahewa Mali, ametangaza katika kituo cha runinga ya kitaifa kuundwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Kuwaokoa Raia (CNSP) ambayo inatarajiwa kuongoza taifa hilo la Afrika Magharibi hadi pale uchaguzi mkuu utapangwa.
“Sisi ndani ya CNSP tunawajibikia raia, lakini pia kuboresha historia ya taifa letu” Wague amelihutubia taifa.
Hatua ya wanajeshi ilijiri baada ya nchi hiyo kukumbwa na mzozo kwa wiki kadhaa upinzani ukiandamana kumtaka Keita kuondoka mamlakani ukimlaumu kwa kuporomosha uchumi na kutoshughulikia ukosefu wa usalama.
Ukosefu wa usalama katika nchi hiyo umesabisha makundi ya kigaidi kukita makao katika eneo la Sahel.
Mnamo Jumanne, viongozi wa upinzani walikusanyika Bamako kuunga wanajeshi huku balozi za nchi tofauti zikionya raia wake kutotoka nje.