Habari MsetoSiasa

Undeni mfumo wa ugavi wa fedha wa kuunganisha taifa -Ruto

August 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto ameitaka kamati maalum ya Seneti iliyoteuliwa kusuluhusha mzozo kuhusu ugavi wa fedha kwa kaunti kubuni mfumo ambao hautaligawanya taifa hili.

Alisema kuwa kamati ya upatanisho sharti ihakikishe kuwa mfumo huo hautaumiza kaunti yoyote wala kufaidi zaidi kaunti zingine, na hivyo kusababisha uhasama nchini.

Akihutubia ujumbe wa wazee na viongozi kutoka kaunti za Bungoma na Trans Nzoia nyumbani kwake Sugoi, kaunti ya Uasin Gishu Ijumaa, Dkt Ruto alisema Seneti ina uongozi hitajika na hekima ya kubuni mfumo ambao unazingatia vigezo vyote muhimu vitakavyowezesha kaunti zote kupata fedha hitajika.

“Kaunti zote ziwe na idadi kubwa ya watu au la zipate haki,” akaeleza.

Kulingana na Dkt Ruto kaunti kama vile Nyeri, Kiambu, Kakamega, Uasin Gishu kati ya zingine zinapasa kupata mgao wao kwa misingi ya idadi ya watu. Na zile zenye watu wachache, akaongeza, kama vile Kwale, Turkana na Mombasa na Kilifi pia zipewe mgao wa kutosha ili miradi ya maendeleo isikwame.

“Kwa kuwa Katiba inahitaji kwamba tubadilishe mfumo wa ugavi wa fedha baada ya miaka mitano, sharti tuhakikishe taifa linasalia kushikamana. Kaunti zenye idadi kubwa ya watu kama Uasin Gishu, Nandi, Kiambu, Nyeri, Kakamega, Kisumu kati ya zingine ziongeweze fedha.

“Lakini pia tuwe waangalifu na tuhakikishe kuwa kaunti kama Vihiga, Tharaka Nithi, Isiolo na Tana River, Mandera, Garissa na nyinginezo hazifai kuumia kwa kupunguziwa fedha zaidi kwa sababu baadhi ya vigezo havikuzingatiwa,” akaongeza.

Dkt Ruto alisema kamati hiyo ya upatanisho, yenye maseneta 12, chini ya uongozi wa Moses Wetang’ula na Johnstone Sakaja, inapasa kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kuchukua msimamo wa pamoja kwa lengo la kuhakikisha taifa limesalia pamoja.

Naibu Rais alisema yeye na Rais Uhuru Kenyatta ni viongozi wa Wakenya wote bila kujali makabila yao, idadi yao au namna walivyopiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Dkt Ruto alieleza kuwa ajenda kuu ya seriali inasalia kuunganisha Wakenya na kufanikisha miradi ya maendeleo sehemu zote nchini.

“Kwa sababu Rais Kenyatta na mimi tunaongoza nchini moja, Seneti inafaa kuhakikisha kuwa imebuni mfumo ambao hautaleta mgawanyiko,” akasema.