• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
ODM yalegeza kamba kwa walioiba fedha za Covid-19

ODM yalegeza kamba kwa walioiba fedha za Covid-19

Mkurugenzi Mkuu wa ODM Oduor Ong’wen. Picha/ Charles Wasonga

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM kimeonekana kuwatetea washukiwa wa ufujaji na uporaji wa pesa za Covid-19 kikisema hawafai kuandamwa kabla ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathangu kutoa ushahidi wa kuwahusisha na uovu huo.

Kwenye kikao na wanahabari Jumamosi, Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna alishuku uhalali wa ufichuzi wa runinga ya NTV kuhusu sakata ya wizi wa Sh43 bilioni zilizotolewa kupambana na janga hilo na ulaghai katika ununuzi wa vifaa vya kinga (PPEs) katika mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (KEMSA).

“Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) haifai kuamriwa kuchunguza sakata katika Kemsa kabla ya ukaguzi wa kina kifanya na Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kubaini uhalali wa madai hayo,” akasema Bw Sifuna katika makao makuu ya ODM, Nairobi.

Alisema bei za PPEs zilikuwa chini kabla ya mlipuko wa Covid-19 kutokea na kwamba bei ya vifaa hivyo vimeongezeka wakati huu kwa sababu vinahitaji kwa wingi kutokana na kupanda kwa visa vya maambukizi.

“Kwa hivyo, bei za juu pekee hazifa kuzingatiwa kama msingi wa kuibua madai kuwa huenda maafisa waliohusika na ununuzi huo walishiriki ufisadi,” akasema Bw Sifuna aliyeandamana na Mkurugenzi Mkuu wa ODM Oduor Ong’wen.

Wiki jana, bodi ya wasimamizi wa Kemsa iliwasimamisha kazi Afisa Mkuu Mtendaji Jonah Manjari, na wakurugenzi Eliud Murithi (Idara ya Biashara) na Charles Juma (Idara ya Ununuzi) kuhusiana na sakata ya ununuzi vifaa vya afya kwa bei ya juu kuliko bei za kawaida.

Kwa mfano uchunguzi wa awali ulibaini kuwa Kemsa ilinunuzi vifaa 10 kwa Sh6,397,034,383 ambavyo vingenunuliwa kwa Sh3,407,512,070.

Mnamo Ijumaa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lililaani ufisadi unaohusishwa na vita dhidi ya janga la corona katika mataifa mbalimbali likifananisha uovu huo na mauaji.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus haswa alitaja ufisadi uliokolea katika mpango wa ununuzi wa vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi (PPEs) akisema unahatarisha maisha ya wahudumu wa afya.

“Ufisadi wowote hautakubalika. Na ufisadi unaohusishwa na PPEs, kwa mtazamo wangu, ni sawa na mauaji. Hii ni kwa sababu ikiwa wahudumu wa afya watafanya kazi bila vifaa hivyo, tunahatarisha maisha yake. Na hiyo pia ni hatari kwa watu wanaowahudumia,” akawaambia wanahabari Ijumaa jijini Geneva, Uswizi.

Dkt Tedro alikuwa akijibu swali kuhusu ufisadi unaohusiana na PPEs wakati huu ambapo vifaa hivyo vinahitajika pakubwa haswa katika mataifa masikini ili vitumiwe na wahudumu wa afya kujikinga.

Ingawa mwanahabari aliyeuliza swali hilo, alikuwa akirejelea madai ya ufisadi yaliyoripotiwa majuzi nchini Afrika Kusini, visa vingine vya ufisadi vimeripotiwa katika mataifa kadhaa Afrika.

Mataifa hayo ni; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zimbabwe, Uganda na Kenya.

Mnamo Ijumaa polisi walikabiliana na makundi ya waandamanaji jijini Nairobi waliokuwa wakishinikiza kukamatwa kwa washukiwa wa sakata ya wizi na ubadhirifu wa fedha za Covid-19.

Na hiyo, jana Rais Uhuru Kenyatta aliamuru DCI kuanzisha uchunguzi kuhusu sakata hizo kwa lengo la kuwakamatwa wahusika na kuwafungulia mashataka kwa mujibu wa sheria.

ODM jana iliitaka Afisa ya Bi Gathungu kutoa ushahidi wa kamili kuhusu sakata hizi ili wahusika wachukuliwe hatua.

“Bila ushahidi kamili kutolewa, habari zinazosambazwa wakati huu kuhusu wizi wa fedha za Covid-19 zinachangia wafadhili kuinyima Kenya fedha za kupambana na janga hili wakati kama huu ambapo visa vya maambukizi vinaongeza,” Bw Sifuna akaonya.

You can share this post!

ODM yamtaka Dkt Ruto ajiuzulu kwa kumkejeli Rais

Young Achievers yaibuka mabingwa