Michezo

Levante yaiharibia Barcelona karamu ya kutoshindwa

May 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MGHANA Emmanuel Boateng aliongoza ‘Daudi’ Levante kuonyesha ‘Goliathi’ Barcelona kivumbi kwa kichapo cha mabao 5-4 mbele ya mashabiki 22 384 uwanjani Valencia, Jumapili.

Ushindi wa Levante ulizima matumaini ya Barcelona kushinda Ligi Kuu bila kupoteza mechi msimu 2017-2018.

Barcelona, ambayo ilikuwa imeshinda mechi 27 na kutoka sare tisa kwenye ligi hii ya klabu 20, pia ilikuwa imepiga Levante mara 19 na kutoka sare mara nne katika mechi 23 zilizopita kabla ya kupigwa breki.

Boateng, ambaye ripoti nchini Ghana zinasema amejumuishwa katika timu ya Black Stars kwa mechi za kirafiki dhidi ya Japan na Iceland, aliingia katika daftari za kumbukumbu kwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga ‘hat-trick’ dhidi ya Barcelona ligini tangu Diego Forlan mwaka 2005.

Levante, ambayo mara ya mwisho ilikuwa imelemea Barcelona ilikuwa 1-0 katika shindano la Copa del Rey Januari 8 mwaka 2004, iliongoza 5-1 dakika ya 56 kupitia mabao ya Boateng yaliyopatikana dakika za tisa, 30, 39 na 49 na mabao mawili kutoka kwa raia wa Macedonia, Enis Bardhi dakika za 46 na 56.

Barcelona ilipata mabao yake kupitia Philippe Coutinho dakika ya 38, 59 na 64 na penalti kutoka kwa Luis Suarez.

Ni mara ya kwanza Barcelona imepoteza mechi ligini katika mechi 44. Kocha Ernesto Valverde atajutia hatua yake ya kutomtumia mchana-nyavu matata Lionel Messi dhidi ya nambari 15 Levante. Ligi Kuu ya Uhispania itatamatika Mei 20.