Habari Mseto

Vyuo vikuu MKU na Leipzig cha Ujerumani, vyafadhili watafiti

August 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya na kila cha Leipzig cha Ujerumani, zimeanzisha ufadhili kwa wanaosomea uzamili na wale wanaendesha utafiti katika uzamifu.

Kulingana na mpangilio uliopo, ni kwamba yeyote anayenuia kupokea ufadhili huo ni sharti awe ni wa umri wa miaka 35 na awe amejisajili rasmi katika mpangilio wa kufanya somo la uzamili. Pia ni lazima awe anaendesha masomo yake katika chuo kinachotambulika rasmi.

Ufadhili huo utakuwa wa Sh54,000 kwa muda wa miezi mitatu lakini hakuna kiwango kingine kitakachotolewa cha kuendesha masomo ya nje.

Mpango huo uko wazi hadi leo Jumatatu Agosti, 24, 2020, na maelezo zaidi yanapatikana katika tovuti ya MKU.

Kwa hiyo, yeyote aliye na mpango wowote wa kuendelea na masomo yake ni sharti awasiliane kupitia tovuti hiyo ya chuo hicho.

Baadhi ya maswala muhimu yanayostahili kutiliwa maanani kwa yeyote anayetaka ufadhili huo ni sharti awe na mwelekeo wa utafiti unaolenga jinsi ya kubuni kazi kibinafsi, hasa kuhusiana na biashara.

Mkenya yeyote wa chini ya umri wa miaka 45 aliyehitimu uzamifu kwa muda wa miaka mitano iliyopita anaruhusiwa kuulizia ufadhili wa fedha hizo kutoka kwa vyuo hivyo viwili.

Aliye katika kiwango hicho atapokea ufadhili wa Euro 600 ambazo ni takribani Sh76,000 fedha za Kenya kwa muda wa miezi mitatu ama minne.

Katika mpangilio huo ubunifu wa kiwango chake unakubalika.

Mkuu wa kitengo cha utafiti katika chuo cha Mount Kenya Dkt Peter Kirira alisema wale wote watakaonufaika na ufadhili huo majina yao yatachapishwa rasmi Septemba 2, 2020.

Alisema Ijumaa, ushirikiano wa pande zote mbili utaendelea kwa maelewano ya kuboresha hali ya elimu ya juu bila ubaguzi.

Alisema lengo kuu la mpango huo ni kuona ya kwamba wasomi wanaafikia malengo yao ambapo baada ya kukamilisha utafiti wao wanafaulu kujiajiri wenyewe kwa juhudi zao na ubunifu.

Kitengo cha German Academic Exchange Service (DAAD), ni shirika ambalo linalenga kuwainua wasomi kielimu na kiuchumi.

Dkt Kirira alisema chuo cha Mount Kenya kinalenga kuwapa mwelekeo wasomi zaidi ili kufanikisha malengo yao katika soko la ajira kote ulimwenguni kwa sababu bara la Afrika lina matatizo ya ajira kwa wahitimu wengi ambapo wasio na ajira ni zaidi ya asilimia 30.

Alisema mradi kama huo pia unaendeshwa katika nchi za Rwanda, Ghana, Tunisia, Benin, na Nigeria ambapo chuo kikuu cha Leipzig cha Ujerumani ndicho mfadhili mkuu.