Makala

TAHARIRI: Ufisadi hautambui mirengo ya kisiasa

August 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

MAJIBIZANO yanayoendelea kati ya chama cha ODM na mrengo wa Naibu Ras Dkt William Ruto kuhusu ufisadi hayana msingi.

Pande hizo mbili zimeendelea kulumbana kuhusu madai ya ufisadi dhidi ya wanaoshukiwa kuiba pesa za kukabiliana na janga la Covid-19.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo na runinga yetu ya NTV ulionyesha kupitia nyaraka kwamba mamilioni ya pesa na vifaa vilinyakuliwa na watu wachache.

Pesa zilizopaswa kuwa marupurupu na mishahara ya madaktari na wahudumu wengine wa afya, za kununua vifaa vya kujikinga, ziliibwa.

Sasa hivi, madaktari na wauguzi katika maeneo mbalimbali ya nchi, wamegoma. Mgomo wao unaeleweka. Baadhi yao wamefanya kazi hiyo ya kuhatarisha maisha, lakini hawajalipwa mishahara tangu Mei.

Kuna wale wanaojitolea kila siku kutoa huduma katika mazingira hatari, ilhali hakuna vifaa vya kujikinga. Hawapo katika mpango wa kupewa usaidizi wa aina yoyote. Wanapitia haya wakati ambapo wenzao kadhaa wamekufa kutokana na Covid-19.

Jambo la msingi kwa kiongozi yeyote sasa linekuwa kuhimiza hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wahusika kwenye kashfa hiyo ya wizi.

Inashangaza kuona chama cha ODM kikitoa taarifa inayofanya kionekane kama kinachowatetea washukiwa.

Kwamba mshukiwa hana hatia hadi korti ithibitishiwe haina maana kuwa watu au mashirika hawawezi kushinikiza kuchukuliwa hatua kwa washukiwa.

Kama kweli taarifa ya NTV kuhusu ufisadi katika shirika la serikali la usambazaji dawa (Kemsa) si ya kweli, basi ni kwa nini kuna viongozi ambao wameondoka?

Inafahamika kwamba viongozi wengi wa ODM ni mawakili na wana haki kuwakilish wateja wao. Lakini uwakilishi huo ufanywe mahakamani na wala si kubadili fikira za wananchi kuhusu suala lenye uzito kama la kuibwa pesa na vifaa vya kukabili Covid-19.

Kwa upande wake, Dkt Ruto na wafuasi wake wanapaswa kukemea ufisadi na wala si kuingiza siasa kwamba ODM wanawalinda washukiwa.

Jambo ambalo pende zote husika zinapaswa kukabiliana nalo ni ufisadi, bila kujali kama aliyeufanya anajihusisha na mrengo gani.

Kwa hivyo, tunaunga mkono hatua ya Mkuu wa Utumishi wa Umma kuagiza afisi za DCI na EACC kuchunguza wizi huo haraka, upesi.