• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:20 AM
Kisumu All Stars sokoni kutafuta kocha mpya na maafisa wa benchi ya kiufundi

Kisumu All Stars sokoni kutafuta kocha mpya na maafisa wa benchi ya kiufundi

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Kisumu All Stars kinachoshiriki Ligi Kuu ya soka ya humu nchini kimetangaza nafasi za kazi katika benchi nzima ya kiufundi.

Nicholas Ochieng ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa klabu hiyo, amesema kwamba wanapania sasa kumwajiri kocha mkuu, mkufunzi msaidizi, kocha wa viungo vya mwili na mkufunzi wa makipa.

Hii ni baada ya All Stars kuagana rasmi na Andrew Aroka (kocha mkuu), Jeff Odongo (kocha wa viungo vya mwili) na Fredrick Onyango (kocha wa makipa) walioteuliwa kuhudumu katika benchi ya kiufundi mnamo Februari 2020.

Aroka ndiye afisa aliyewahi kuhudumu kambini mwa kikosi hicho kinachodhaminiwa na Serikali ya Kaunti ya Kisumu kwa muda mrefu zaidi na ndiye aliyechangia zaidi kupandishwa ngazi kwa kikosi hicho kushiriki soka ya Ligi Kuu mwanzoni mwa msimu huu wa 2019-20.

Mnamo Januari 2020, All Stars walimtimua aliyekuwa kocha wao wa muda mrefu, marehemu Henry Omino kwa pamoja na aliyekuwa msaidizi wake, Aroka na kocha wa makipa Joseph Ongoro kwa sababu ya matokeo duni ya kikosi.

Hata hivyo, Aroka alirejea baadaye kambini mwa klabu hiyo baada ya Arthur Opiyo aliyeteuliwa kushikilia mikoba ya kikosi hicho kwa muda kurejea nchini Ujerumani kwa mafunzo zaidi ya ukocha.

Kwa mujibu wa Ochieng, waliokuwa vinara wa kikosi hicho, wakiwemo Aroka, Odongo na Onyango wako huru kutuma upya maombi ya kazi kwa minajili ya kujaza nafasi ambazo sasa zimetangwa ziko wazi.

“Walikuwa wametia saini mikataba ya miezi michache ambayo kwa sasa imekatika. Wako huru kuwasilisha upya maombi yao kwa minajili ya kuendelea kuhudumu nasi katika benchi mpya ya kiufundi ambayo tunapania kuifichua rasmi mwanzoni mwa Septemba,” akasema Ochieng kwa kusisitiza kwamba wanamtafuta kocha mkuu aliye na leseni ya kiwango cha C kutoka kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Benchi mpya ya kiufundi itakayoundwa na All Stars itakuwa na kibarua cha kwanza cha kuongoza kikosi hicho kuvaana na Vihiga United kwenye mechi za mikondo miwili ya kubaini klabu ya ziada itakayoshuka daraja kwenye Ligi Kuu ya FKFPL na kitakachopanda ngazi kutoka Betika NSL kwa minajili ya kinyang’anyiro cha msimu mpya wa 2020-21.

Kisumu All-Stars walishikilia nafasi ya 16 kwenye jedwali la KPL mnamo 2019-20 huku Vihiga United wakimaliza kampeni za NSL katika nafasi ya tatu nyuma ya Bidco United na Nairobi City Stars.

You can share this post!

LISHE: Keki ya ‘pundamilia’

AK kufanyia wanariadha 230 majaribio kabla ya kuwachuja kwa...