MUDAVADI: Sina nia ya kuwa mgombea mwenza wa yeyote mbio za Ikulu 2022
Na SAMMY WAWERU
KIONGOZI wa ANC Musalia Mudavadai amesema hatakuwa mgombea mwenza wa yeyote kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ambao inatarajiwa utaandaliwa mwaka 2022.
Amesema umewadia wakati ambapo viongozi aliounga mkono hapo awali kuwania urais wanafaa “warejeshe mkono”, akisema ana imani ya kuleta taifa pamoja na kukwamua uchumi.
Bw Mudavadi alisema, 2022 lazima awe debeni kama mwaniaji wa urais. ANC ni kati ya vyama vilivyounda muungano wa Nasa kuwania urais 2017, ambapo kiongozi wa ODM Raila Odinga ndiye alipeperusha bendera.
Aidha, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alikuwa mgombea mwenza wa Raila. Vyama vingine vilivyounda muungano wa Nasa, na ambao kwa sasa umeonekana kusambaratika ni pamoja na Ford – Kenya, kinachoongozwa na seneta wa Bungoma Moses Wetangula na Chama Cha Mashinani, cha aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Rutto.
“Uchaguzi wa 2022 sitakuwa mgombea mwenza wa yeyote akiwemo Raila ikiwa atawania urais kwa sababu nami pia nitakuwa debeni,” Mudavadi akasema.
Alisema hayo kwenye mahojiano na runinga ya Citizen.
Alipoulizwa iwapo anaweza kushirikiana na kiongozi wa ODM Raila Odinga, Makamu huyo wa Rais zamani alisema “akiamua na kukubali kuwa mgombea mwenza wangu, nitamkaribisha”.
Wengine waliotangaza nia kuwania urais 2022 ni pamoja na Naibu wa Rais Dkt William Ruto, Kalonzo Musyoka, na Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua ambaye pia ni kiongozi wa Maendeleo Chap Chap.
“Naibu Rais Ruto yuko debeni kuwania urais, sitakuwa mgombea mwenza wake. Ni mshindani wangu,” Bw Mudavadai akasema.
Hatma ya Raila Odinga kuwania urais 2022 haijajulikana, Waziri huyo Mkuu wa zamani akisema kwa sasa anashirikiana na Rais Uhuru Kenyatta kuunganisha taifa, kufuatia mkataba wao wa makubaliano wa Machi 2018, almaarufu Handisheki.
Hata hivyo, wandani wake wanahoji Bw Raila atakuwa debeni kuwania urais 2022, ushirikiano wake wa karibu na Rais Kenyatta ukisemekana ni njia ya kumuingiza Ikulu.
Baadhi ya wanasiasa na viongozi wa eneo la Magharibi hasa wanaohusishwa na mrengo wa ‘Tangatanga’, unaoegemea upande wa Dkt Ruto umekuwa ukishinikiza Mudavadi ajiunge na merikebu ya Naibu wa Rais, wakimsihi awe mgombea mwenza.