Michezo

USM Alger yatua nchini kukabiliana na Gor Confederations Cup

May 15th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

VIONGOZI wa Kundi D, USM Alger wametua jijini Nairobi tayari kupambana na Gor Mahia katika mechi ya Kombe la Mashirikisho (Confederations Cup).

Alger, ambayo ilifungua mechi za makundi kwa kupepeta Young Africans (Yanga) kutoka Tanzania 4-0 Mei 6, ilitoka nchini Algeria saa tisa alasiri Jumapili na kupumzika jijini Doha nchini Qatar kwa saa mbili na nusu kabla ya kuendelea na safari hadi Nairobi.

Mabingwa hawa mara saba wa Algeria watavaana na mabingwa mara 16 wa Kenya, Gor, Jumatano saa moja usiku katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.

Klabu hizi hazijawahi kukutana katika historia yao. Alger, ambayo ilifika nusu-fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2017 na fainali ya kombe hilo mwaka 2015, inatarajiwa kuwa na vipindi viwili vya mazoeziuwanjani Kasarani kabla ya kumenyana na Gor.

Timu hizi zilijiandaa kwa mchuano huu kwa kupoteza mechi zao. Alger ilizabwa 3-2 na JS Kabylie hapo Mei 11 katika mechi ya Ligi Kuu ya Algeria nayo Gor ikalemewa na Hull City kutoka Uingereza 4-3 kwa njia ya penalti katika mechi ya kirafiki uwanjani Kasarani mnamo Mei 13.

Alger inaongoza Kundi D kwa alama tatu ikifuatiwa kwa karibu na Gor na Rayon Sport ya Rwanda (alama moja kila mmoja) nayo Yanga inavuta mkia bila alama.