• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
CYNTHIA KASIDI: Nipe miaka mitano, nitakuwa mwigizaji bomba

CYNTHIA KASIDI: Nipe miaka mitano, nitakuwa mwigizaji bomba

Na JOHN KIMWERE

ANAAMINI anacho kipaji cha kufanya vizuri katika tasnia ya maigizo na kutwaa tuzo za kimataifa kama Oscars na Grammys kati ya zingine. Mwigizaji huyu anasema anapania kujituma mithili ya mchwa ili kutimiza ndoto zake ikiwamo kukuza talanta za wasanii wanaoibukia.

Anadokeza kuwa analenga kufuata nyayo za waigizaji mahiri duniani kama Taraji Penda Henson maarufu Cookie mzawa wa Marekani. Msanii huyo alijizolea sifa tele kutokana na filamu zake maarufu kama ‘What men want,’ na ‘Koffee and Kareem’ kati ya zingine. Cynthia Khavesta Kasidi ni miongoni mwa waigizaji wanaoibukia wanaopania kufikia hadhi ya kuigiza katika filamu za kimataifa (Hollywood) ndani ya miaka michache ijayo.

SUMU LA PENZI

Binti huyu ni mwanafunzi wa mwaka wa pili kwenye Chuo Kikuu cha East Africa Institute of Certified Studies (ICS) anakosomea kuhitimu kwa shahada ya Diploma katika masuala ya Uhusiano Mwema.

”Nilianza kujituma katika masuala ya maigizo muda tu nilipomaliza elimu ya Shule ya Upili kwenye Shule ya Lirhanda Girls mwaka 2017,” alisema na kuongeza kwamba mwaka mmoja baadaye alivutiwa zaidi na uigizaji baada ya kutazama kipindi cha Sumu la Penzi.

”Ingawa nimegundua uigizaji sio jambo rahisi ninataka kukaza buti nihakikishe nimetinga upeo wa kimataifa hivi karibuni,” alisema na kuongeza kuwa anamwomba Mungu zaidi ili amwezeshe kupiga hatua katika masuala ya maigizo. Binti huyu aliyezaliwa mwaka 1998 katika eneo la Khaega, Kaunti ya Kakamega anajivunia kushiriki filamu nyingi tu ingawa hazijafaulu kuonyeshwa kwenye runinga yoyote nchini.

Baadhi ya filamu hizo zikiwa ‘Black Wedding,’ ‘Opiyo has risen,’ ‘Razors,’ ‘The Evidence,’ na ‘Who will marry her,’ kati ya zingine. Licha ya filamu hizo kutopata mwanya kuonyeshwa kwenye runinga anaamini kwamba ipo siku milango yake itakapofunguka na mambo kuwa shwari katika usanii wake.

MIAKA MITANO

Kwa jumla msichana huyu anajivunia kufanya kazi ya filamu chini ya makundi mbali mbali kama Starlite Production, Millaz Production, Elite, Epitome production kati ya zingine. Kipusa huyu aliyedhamiria kuhitimu kuwa mwana sheria kabla ya matamanio yake kwenda mrama anasema ndani ya miaka mitano ijayo analenga kuwa mwigizaji anayetambulika nchini.

Chipukizi huyu anasema kuwa kwa wasanii wachache hapa nchini ambao angependa kufanya kazi nao ni kama Brenda Wairimu ‘Selina’ na Serah Ndanu ‘Sumu la Penzi.’ Kisura huyu anayeamini usanii ni ajira kama nyingine anasema serikali inastahili kuwekeza zaidi katika tasnia ya uigizaji ili kusaidia chipukizi wanaokuja- wavulana na wasichana.

USHAURI

Ingawa hajapata mashiko anashauri waigizaji wanaoibukia kuwa kamwe wasife moyo wala wasiwe na pupa ya kupata umaarufu bali nyakati zote wamtumainie Mungu kwa chochote wanachofanya.

Aidha anasema wanastahili kuwa wabunifu, wajifunze kujituma mzigoni pia wajiamini wanatosha mboga katika kazi zao. Pia anawashauri kuwa wanapaswa kufuata mwelekeo unaofaa wala wasikubali kushushwa hadhi na maprodusa mafisi.

You can share this post!

CHRISTINE NJERI: Napania kutinga upeo wa Jenniffer Lawrence

JACK OCHIENG: Kocha nguli nchini na Afrika Mashariki