Habari

RUTO: Walioiba pesa za corona wajiuzulu upesi

August 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU Rais William Ruto anataka wakuu serikalini waliohusika na wizi wa fedha zilizotengwa kukabiliana na janga la virusi vya corona kuondoka afisini kwa muda kupisha uchunguzi.

Naibu wa Rais pia amepinga vikali pendekezo la kiongozi wa ODM Raila Odinga kutaka mhasibu mkuu wa serikali kufanya uchunguzi ili kubaini fedha zilizopotea.

Alisema Wakenya wanataka kujua kwa nini Bw Odinga anataka mhasibu mkuu kuchunguza sakata hiyo ilhali kuna taasisi huru za kupambana na ufisadi.

“Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) na Afisi ya Mashtaka ya Umma (DPP) hazifai kungojea mkaguzi wa hesabu za serikali,” akasema Dkt Ruto.

Inadaiwa kuwa watu wenye ushawishi serikalini walijipatia tenda za kusambaza vifaa vya kukinga wahudumu wa afya dhidi ya virusi vya corona, maarufu PPEs, kutoka kwa Shirika la Kusambaza Vifaa vya Matibabu (Kemsa).

Wafanyabiashara hao waliuzia serikali vifaa hivyo kwa bei maradufu hivyo kusababisha nchi kupoteza mabilioni ya fedha.

“Mbona wakuu serikalini waliohusika katika sakata hiyo hawajawajibika kwa kujiondoa kwa muda kupisha uchunguzi? Kwanini kampuni zilizohusika hazijachunguzwa? Mbona hawajakamatwa na kufikishwa kortini? Labda ni kwa sababu walioiba fedha za corona si wandani wa Naibu wa Rais Ruto,” akasema Naibu wa Rais.

Dkt Ruto, wiki iliyopita, alimkejeli Rais Uhuru Kenyatta huku akisema hatamlaumu kwa kupotea ya mabilioni ya fedha kwani hajahusishwa katika juhudi za kukabiliana na janga la virusi vya corona humu nchini.