Makala

Mazishi ya dakika 20 ya aliyekuwa kinara wa 'Mungiki'

August 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA kinara wa kundi haramu la Mungiki ukanda wa Kati ya Mlima Kenya kati ya 2001 na 2008 Mwangi wa Njoki alizikwa Jumanne chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa polisi katika Kaunti ya Murang’a.

Katika enzi zake za kutesa na kundi hili haramu ambalo lilisambaratishwa na juhudi na harakati kali za aliyekuwa Waziri wa Usalama John Njoroge Michuki mwaka wa 2007, marehemu alikuwa katika ngazi ya ‘Mkuu wa Mkoa’ (PC).

Kundi hili lilikuwa na mpangilio wa kiafisi sawa na ule wa utawala wa serikali kuu ambapo kileleni lilikuwa na kiongozi wao Maina Njenga (ambaye kwa sasa amekiri kurekebisha mienendo na kuokoka katika imani ya Kikristo) na aliyekuwa akiongoza naibu wake na nyanjani akiwa na wakuu wa mikoa, wilaya, tarafa, lokesheni na kata.

Takriban maafisa 250 wakiabiri magari rasmi na ya kibinafsi, wakiwa wamevalia sare rasmi na wengkine wakivalia kiraia lakini wote wakiwa wamejihami vikali, walilazimisha mazishi hayo kumalizika chini ya muda wa dakika 20.

Maafisa wengine waliandamana na waombolezaji hadi hifadhi ya maiti ya Murang’a wakifuatilia hali na kuwapasha habari wenzao waliokuwa wameshika doria katika maeneo kadhaa ya mji wa Maragua na ambapo kulikuwa na vizuizi vitano vya kupiga msasa waliokuwa wanalenga kuhudhuria mazishi hayo.

Ni operesheni ambayo iliishia kukamatwa kwa washukiwa 15 na pikipiki zaidi ya 30 zikanaswa huku waendeshaji na walioziabiri wakitoweka.

Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kusini Anthony Keter alisema kuwa hatua hiyo iliafikiwa baada ya habari za ujasusi kufichua kwamba kulikuwa na njama ya waliokuwa wafuasi wa kundi hilo kujitokeza katika mazishi hayo na kuvuruga amani.

“Pia Februari tulikuwa na mazishi ya bintiye marehemu ambaye aliuawa jijini Nairobi kama mshukiwa wa kundi la uhalifu la Gaza. Vijana waliojitokeza katika maziko hayo walivuruga amani ya mji wa Maragua kwa kiwango kikuu na wao pia walikuwa wanalenga kurejea tena katika mazishi hayo ya jana Jumanne, hali ambayo hatungekubali kamwe,” akasema.

Ni mazishi yaliyowaacha wenyeji vinywa wazi kwa kuwa licha ya mapochopocho kuandaliwa na kuwekwa tayari kwa waombolezaji, polisi waliwazima kujivinjari na pia kukawa hakuna misa wala kusomwa kwa historia ya maisha ya marehemu.

Maafisa walitoa amri kwanba ni vizuri stori nyingi zikatwe na mwili uzikwe mara moja.

Maafisa wa polisi waliovalia kiraia walijitokeza katika hifadhi ya wafu ya Murang’a ambapo mwili wa mwendazake uliondolewa mwendo wa saa tatu na nusu asubuhi, jeneza lililoubeba likapakiwa katika gari la huduma za wafu la Lossalina na kuanza mwendo wa kuelekea katika eneo la mazishi chini ya ulinzi fiche wa maafisa hao.

Kufika katika kiingilio cha mji wa Maragua katika barabara kuu ya Murang’a hadi Nairobi maafisa walikuwa wameweka kizuizi kilichokuwa chini ya uongozi wa Bw Keter akishirikiana na maafisa wa kitengo cha ujasusi na pia uchunguzi wa jinai (DCI) huku machifu na manaibu wao wakiwa nyanjani wakipiga msasa waombolezaji waliokuwa na nia ya kujitokeza.

Mwili ulifika katika boma lake saa nne na dakika thelathini na tano asubuhi na saa tano kasoro dakika 10 mwili ulikuwa ndani ya kaburi huku vijana wakiagizwa warejeshe mchanga kuufunika nao maafisa wa polisi wakishika doria.

Waombolezaji wengine walikuwa tayari wameamrishwa waondoke eneo hilo kwa kuwa shughuli ya kuhuzunikia karibu na mahala hapo ilikuwa imeisha.

Maafisa wa polisi waziba lango la kuingia pale alizikwa aliyekuwa kinara wa ‘Mungiki’ ukanda wa Kati, Mwangi wa Njoki katika kijiji cha Mathare, Murang’a, Agosti 25, 2020. Picha/ Mwangi Muiruri

Maafisa wengine walikuwa wametangamana na raia kwa kuwa kulikuwa na fununu kwamba kulikuwa kujitokeze waombolezaji hatari wenye misimamo mikali kutoka kundi la Mungiki na lile la Gaza.

Mnamo Februari, bintiye mwendazake aliuawa katika kisa cha adhabu ya kitutu jijini Nairobi kwa madai ya kuwa mfuasi wa Gaza na ambapo mazishi yake yalichafua mji wa Maragua kupitia kujitokeza wakora waliohangaisha wenyeji huku wakivuta bangi hadharani na kutumia lugha chafu dhidi ya maafisa wa kiutawala na pia wenyeji.

“Hayo ndiyo matarajio yetu ambayo yalituchochea kufika eneo hilo na kuthibiti hali. Hakuna haja ya sisi kudanganyana hapa kuwa hafla hii ilikuwa ya kawaida. Ni mazishi yaliyojaa hatari kwa usalama wa eneo,” akasema Bw Keter.

Alisema kuwa serikali haiwezi kuwa imechanganyikiwa kiasi cha kupoteza muda wake kupanga operesheni kubwa kiasi hicho ikiwa haina habari za uhakika kuhusu hatari.

Licha ya wandani wa familia hiyo kusisitiza kwamba mwendazake alikuwa mtiifu na aliyekuwa amerekebisha mienendo, maafisa walisema shida haikuwa maiti bali waombolezaji.

Aliyekuwa Naibu kamanda wa Polisi wa Makuyu Jasper Makau aliambia Taifa Leo kuwa mwendazake alikuwa hatari sana wakati alikuwa mfuasi wa ‘Mungiki’.

“Nilimkamata mwaka wa 2004 akiwa na wengine wanne ambapo shutuma dhidi yao ilikuwa kutekeleza mauaji, utozaji haramu wa ushuru, kutishia maisha ya wengine na kuongoza hafla za kiapo kwa makurutu wa Mungiki,” akasema.

Anasema kuwa baada ya kuwafikisha katika mahakama ya Kigumo, kesi ilianguka kwa kuwa mashahidi walihepa wakihofia maisha yao.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Murang’a Mashariki (kabla ya nyadhifa hizo kufutiliwa mbali na Katiba Mpya 2010) George Natembeya ambaye kwa sasa ni mshirikishi wa usalama Rift Valley aliambia Taifa Leo kuwa “huyu Mwangi wa Njoki namkumbuka vyema akiwa sura ya ‘Mungiki’ eneo hilo nikihudumu Murang’a.”

Natembeya ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa DC alikuwa msaidizi wa Michuki katika jumba la Harambee House alisema: “Namkumbuka akiwa na msaidizi wake aliyefahamika kama Mbau na ambaye pia ni marehemu kwa sasa baada ya kulimwa risasi na maafisa wa polisi.”

Alisema kuwa kabla ya marehemu Mwangi wa Njoki kujiunga na Mungiki, alikuwa muuzaji chang’aa katika mtaa wa Mathare.

“Hayo ni kabla ya kulegeza mbio zake za kimaisha na kuanza kuuza matunda na mboga katika mji wa Maragua. Naelewa kuwa shida haikuwa kuhusu historia yake ya ujambazi bali washirika ambao walipanga kuhudhuria mazishi hayo. Serikali ina wajibu wa kuzima hatari zote kabla ya zitokee na ndiyo sababu raia huhimizwa wapige ripoti za mapema kuhusu hatari za kiusalama serikali iziwajibikie kabla ya hazijasababisha kilio kwa jamii,” akasema.

Kamishna wa Murang’a Mohammed Barre alisema kuwa “tuko pia na janga la Covid-19 ambalo ni wajibu wetu kulizima makali” na ambapo mikusanyiko yote haramu na hatari imezimwa.

“Maafisa wangu pia walijitokeza kupiga msasa hafla hiyo ya mazishi na kwa sasa tunafaa kuzingatia changamoto zetu za kimaisha ambazo ziko mbele yetu,” akasema Barre.

Alisema kuwa wenyeji wa eneo hilo hawatakuwa na budi kushuhudia doria sawa na hizo zilizoshuhudiwa Maragua katika hali zote ambazo utathmini wa vitengo vya usalama utafichua njama hatari kwa usalama wa eneo.