• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
TAHARIRI: Magoha aache kuyumbayumba

TAHARIRI: Magoha aache kuyumbayumba

Na MHARIRI

HUKU wazazi wakingoja kwa matumaini kufunguliwa kwa shule nchini ili watoto wao warejelee masomo mnamo Januari, matamshi ya Waziri wa Elimu Profesa George Magoha yameendelea kuwakanganya wadau wa sekta hii wakiwemo walimu.

Akiwa katika ziara ya kukagua Chuo anuwai cha Kisii jana Jumanne, waziri Magoha alisema serikali inaendelea kushauriana kuhusu ni lini na vipi shule zitafunguliwa huku akionya wale wanaosukuma shughuli hii ya ufunguzi.

Magoha alitaja wakora na shule za binafsi kama wahusika wanaotilia presha zaidi utelezwaji wa zoezi hili.

Akiwa kwenye kikao na wabunge majuzi, Waziri alisema kwamba hana uhakika kuhusu ni lini shule zitarejelewa. Alinukuliwa akisema kuwa ni Rais Uhuru pekee atayetangaza wakati mwafaka wa watoto kurudi masomo.

Wazazi wengi humu nchini wana hamu ya kuwaona wanao wakiwa shuleni huku baadhi ya wengine wakihofia maambukizi ya corona yanayoendelea kushuhudiwa nchini.

Kundi moja linapendekeza maambukizi yadhibitiwe na chanjo la kuzuia corona kupatikana kwanza huku lile lingine likipuuza msimamo huo.

Wiki iliyopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilishauri nchi za Afrika zianze mikakati ya kurejesha watoto shuleni kuepuka madhara makubwa yanayoweza kusababishiwa watoto kutokana na kuwa nje ya shule kwa muda mrefu.

Kufikia sasa, nchi kadhaa barani zimefungua taasisi zao Afrika Kusini ikiwa ya hivi karibuni kutekeleza hili. Baadhi ya nchi zingine ni majirani Tanzania, Uganda na Burundi. Rwanda inapanga kutuma wanafunzi shuleni mwezi ujao.

Hata ingawa mpango wa masomo ya kijamii mashinani umezinduliwa na serikali sasa, kuna tashwishi kadha ambazo zinakumba mradi huo ikiwemo dai kwamba ni wanafunzi wachache tu ambao watafikiwa. Pia, kuna tetezi kwamba masomo yanaoendeshwa hayana faida ya haja kwa wanafunzi wanaolengwa.

Baadhi ya walimu wameokana kulegea kukumbatia mpango huu.

Ni jukumu la wizara kutoa mwelekeo kamili kuhusu msimamo wake rasmi wa ratiba ya masomo nchini ikizingatia sera zake.

Kwa hivyo Profesa anafaa kutoa uamuzi wa serikali ili kumaliza shaka na mahangaiko yanayokumba wazazi na watoto wao.

Magoha atekeleze wajibu wake bila kutatarika kwa kurejelea tajriba yake kama msomi.

You can share this post!

Mazishi ya dakika 20 ya aliyekuwa kinara wa...

ODONGO: Kauli ya Raila kuidhinisha Nyong’o ugavana...