• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
GWIJI WA WIKI: Shullam Nzioka

GWIJI WA WIKI: Shullam Nzioka

Na CHRIS ADUNGO

PANIA kuwa bora katika chochote unachoteua kukishughulikia.

Likichomoza, liote! Kwa kuwa Mola ndiye mwelekezi wa hatua zote tunazozipiga maishani, inatulazimu kumweka mbele siku zote.

Kufaulu katika jambo lolote kunahitaji mtu kuwa na maono. Nidhamu, bidii, uvumilivu na imani ni kati ya mambo muhimu yanayochangia mafanikio ya binadamu. Jitume ili upate matokeo bora.

Kila binadamu ana kipaji ambacho ni wajibu wake kukitambua na kutia azma ya kukipalilia. Huwezi kujiendeleza maishani iwapo hujiamini.

Amini kwamba unaweza na usichoke kutafuta. Usilie wala kukata tamaa usipofaulu. Endelea kujikaza na milango ya heri itajifungua yenyewe.

Hatua ya kwanza katika safari yoyote ya ufanisi ni kufahamu kile unachokitaka; kujielewa wewe ni nani na kutambua mahali unapoenda.

Huu ndio ushauri wa Bw Shullam Nzioka – mwandishi wa Fasihi ya Kiswahili na mhubiri ambaye kwa sasa ni Mratibu wa Idara ya Huduma katika kampuni ya Armco Kenya Ltd, Embakasi, Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Shullam Nzioka alizaliwa mnamo 1980 mjini Kitale, Kaunti ya Trans-Nzoia. Yeye ni mwana wa pili katika familia ya Bw Kituku Nzioka na Bi Margaret Nzioka.

Alianza safari ya elimu katika Shule ya Kilimani Police Nursery, Nairobi kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Mbagathi Road, Nairobi mnamo 1986. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwishoni mwa 1993.

Alifaulu vyema na kupata nafasi ya kusomea katika Shule ya Upili ya Upper Hill, Nairobi mnamo 1994. Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mwishoni mwa 1997.

Nzioka anatambua ukubwa na upekee wa mchango wa baba yake mzazi katika ufanisi anaojivunia kwa sasa katika ulingo wa Kiswahili. Zaidi ya kuwa mwalimu wake wa awali maishani, Bw Kituku alimhimiza mno ajitahidi masomoni.

Baada ya kubaini utajiri wa kipaji cha mwanawe katika uandishi wa kazi za ubunifu, Bw Kituku ambaye aliwahi kuwa mtafsiri wa International Bible Students Association (IBSA), Nairobi, alimpa Nzioka majukwaa mbalimbali ya kuikuza talanta yake.

Aliipalilia sanaa hiyo iliyoanza kujikuza ndani ya Nzioka katika umri mdogo kwa kumnunulia vitabu vya hadithi na nakala ya kila siku ya gazeti la Taifa Leo na Taifa Jumapili.

Walimu pia walimteua Nzioka mara kwa mara kusoma vifungu vya Ufahamu wa Kiswahili na somo la Kiingereza darasani na wakampa nafasi maridhawa ya kuhutubu gwarideni kila Jumatatu na Ijumaa.

Kati ya walimu waliomchochea sana kukipenda Kiswahili akiwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Mbagathi Road, ni Bi Kitaka aliyekuwa mwalimu wake wa darasa kati ya 1986 na 1989.

Chini ya uelekezi wa Bi Kitaka, Nzioka alishiriki mashindano mengi ya kutoa hotuba, akawa gwiji wa ulumbi, na akajizolea tuzo za haiba kubwa.

Ilhamu yake katika utetezi wa Kiswahili ilichangiwa zaidi na Bi Mwangi na Bi Alufa – walimu waliomtanguliza vyema katika somo la Fasihi ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya Upper Hill.

KAZI

Mnamo Mei 1998, Nzioka aliajiriwa kuwa afisa wa kupokea wageni katika kampuni ya kuuza magari ya Prozy Auto Consultants, Nairobi. Alihudumu huko hadi Oktoba, 2000.

Katika kipindi hicho, alikuwa pia akisomea masuala ya kompyuta katika Chuo cha Graffins, Nairobi. Alifuzu Novemba 2000 na kujiunga na IBSA, Nairobi.

Akiwa IBSA, Nzioka alipata mafunzo ya dini na malezi ya ziada ya kiakademia. Alitandikiwa zulia zuri la kujifunza Kiswahili na Kiingereza kwa upana zaidi; na kiwango chake cha umilisi wa lugha kikaimarika na kuboreka mno.

Nzioka alihudumu katika Idara ya Tafsiri ya IBSA kwa kipindi cha miaka minane. Alijishughulisha sana na kazi ya kutafsiri machapisho mbalimbali ya dini kupitia vipeperushi, broshua, kabrasha, majarida na vitabu kutoka Kiingereza hadi Kiswahili.

Aliondoka IBSA mnamo Disemba 2008 na kuwa dereva wa teksi jijini Nairobi. Aliifanya kazi hii kwa kipindi cha miaka miwili kati ya 2009 na 2010.

Ilikuwa hadi mwanzoni mwa 2011 ambapo aliajiriwa na kampuni ya Armco Kenya Ltd katika eneo la Embakasi, Nairobi kuwa Mratibu wa Shughuli katika Idara ya Huduma. Huko ndiko aliko hadi sasa.

UANDISHI

Nzioka anakiri kwamba marehemu Profesa Ken Walibora ndiye alimpigia mhuri wa kuwa mwandishi mzuri wa Kiswahili baada ya kupitia miswada ya kazi zake za kwanza mnamo 2009.

Kwa wakati huo, Prof Walibora alikuwa mhadhiri msaidizi katika Idara ya Lugha za Kiafrika ya Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, Amerika. Kupitia mawasiliano ya barua-pepe, alimtia Nzioka motisha ya kuanza kupiga mbizi katika bahari ya utunzi wa vitabu vya Fasihi.

Baada ya Oxford Publishers kumfyatulia riwaya Si Kitu mnamo 2013, Nzioka aliandika hadithi fupi tatu Hamnazo, Babu ya Majuto na Kijiji cha Matambara zilizochapishwa na kampuni ya Queenex Publishers mnamo 2016.

Mnamo 2018, Queenex ilimtolea riwaya Kipepeo Malidadi kabla ya Oxford kumchapishia riwaya Mbona Hivi? mnamo 2019 kisha hadithi fupi Shani ya Saa katika mkusanyiko wa Utashi wa Dola na Hadithi Nyingine mnamo 2020.

Nzioka kwa sasa anaandaa miswada zaidi ya tamthilia, riwaya na hadithi fupi huku akitazamia kutambua, kukuza na kulea vipaji vya vijana wanaoibukia kwa kasi katika ulingo huu wa uandishi wa kazi bunilizi.

JIVUNIO

Anapojitahidi kuweka hai ndoto ya kuwa mwandishi maarufu wa vitabu, Nzioka anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wapenzi wa Kiswahili ambao wametangamana naye katika makongamano na warsha mbalimbali za makuzi ya lugha.

Nzioka amekuwa pia mhubiri wa Kanisa la Mashahidi wa Yehova (Jehovah’s Witnesses) katika eneo la Mowlem Mashariki, Nairobi tangu 1993.

Anamstahi sana mkewe Bi Philes Mueni ambaye amekuwa nguzo muhimu katika juhudi zake za kukichapukia Kiswahili.

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Shida huzunguka, leo kwangu kesho yaweza...

Beki Harry Maguire aondolewa kwenye timu ya taifa ya...