Balala asisitiza ni sharti Watanzania wawekwe karantini wanapowasili nchini Kenya
Na WINNIE ATIENO
WAZIRI wa Utalii na Wanyamapori, Najib Balala amesisitiza kwamba raia wa nchi ambazo Kenya inaziona ziko katika hatari ya maambukizi ya corona – ikiwemo Tanzania – watawekwa karantini ya lazima wanapowasili humu nchini.
Waziri Balala alisema raia hao watawekwa karantini ya lazima ya siku 14 kulingana na mwongozo wa Shirika la Afya Duniani.
Waziri huyo alisema Kenya itaendelea kudumisha usalama wa watalii katika juhudi za kuimarisha sekta ya utalii.
Wakati huo huo, Bw Balala alisema nchi za Kenya na Tanzania zinaendelea na mazungumzo kabambe ili kuanzisha usafiri wa ndege zao za kitaifa za Kenya Airways na Precision Air ili ziwe zinakubalika kutua na kupaa katika anga ya kila mojawapo ya mataifa haya mawili.
Nchi hizo zimekuwa kwenye mgogoro ambao kwa kiasi kikubwa unahusu janga la virusi vya corona.
Tanzania imekuwa ikisisitiza inakabiliana na janga hilo jinsi inavyostahili.
Bw Balala alisema mipaka ya Kenya ingali imefungwa lakini watalii wanaoingia humu nchini kupitia viwanja vya kimataifa vya ndege ni sharti wafuate kanuni za afya ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.
“Mipaka yetu ya chini ya ardhi bado imefungwa lakini viwanja vyetu vya ndege viko wazi kwa watalii wa humu nchini na wale wa kimataifa. Lakini tuna aina mbalimbali ya wageni; kuna wale wanaotoka nchi hatari zaidi, katikati na wale ambao wanatoka sehemu ambayo iko shwari. Wale wanaotoka nchi ambayo imetajwa hatari na shirika la afya duniani watawekwa karantini ya lazima wka siku 14, ” alisisitiza Bw Balala ambaye alikuwa akijibu maswali kutoka kwa wawekezaji wa sekta hiyo mtandaoni.
Mwekezaji mmoja aliuliza endapo watanzania wanaruhusiwa kuingia nchi ya Kenya kupitia mpaka wa Namanga, hata hivyo waziri huyo alisisitiza kuwa Kenya ingali imefunga mipaka yake.
Kwenye mkutano huo wa wawekezaji wa utalii kutoka nchi za Kenya, Rwanda, Tanzania miongoni mwa zengine walijadili namna ya kuimarisha sekta hiyo wakati wanapokabiliana na janga hilo.
“Tunaweka mikakati kuhakikisha ndege za Precision Air na Kenya Airways zinarejelea safari zao nchi hizo mbili za Kenya na Tanzania,” alisisitiza Bw Balala.
Hata hivyo, mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Utalii nchini Tanzania Devota Mdachi alisema nchi yake haina haja ya kuweka wageni kwenye karantini bora wawe na sakabadhi halali za kuonyesha walipimwa na hawana virusi hivyo.
“Tunaweka mikakati ya kuimarisha sekta ya utalii. Tunafurahi kwamba wawekezaji katika sekta binafsi wameanza kuvutia wageni wa humu nchini kwa kuweka mikakati kabambe ikiwemo bei au ada nafuu,” alisisitiza.
Bi Mdachi alisema Mei 2020 mbuga ya kitaifa ya wanyama wa porini ya Serengeti ilipokea wageni 20 wa kitaifa lakini Julai zaidi ya watalii 270 walimiminika katika sehemu hiyo kuangalia nyumbu wakivuka kutokea mbuga ya Maasai Mara nchini Kenya.
“Tanzania ina hadithi ya kuwaelezea dunia na walimwengu namna tulivyosimama wima ili kuhakikisha afya ya raia wetu na usalama wao. Jopo maalum liliundwa ili kuweka mikakati kabambe, shule zikafungwa tukahamasisha umma namna ya kuishi na virusi hivi,” alisema.