Siasa

Wanasiasa wa mrengo wa Ruto wasema wana mkakati wa kumzamisha Raila

August 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

‘MAJENERALI wa nyanjani’ wa kumpigia debe Naibu Rais Dkt William Ruto katika ukanda wa Mlima Kenya sasa wanasema wanatamani sana mpinzani wao mkuu 2022 awe kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Kwa mujibu wa mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, mpambano wa Dkt Ruto na Bw Odinga katika ushindani wa 2022 ni kinyang’anyiro tosha “lakini cha sisi kumzidi maarifa kiongozi wa ODM.”

“Kwa sasa kuna udhaifu tele katika uwaniaji wa Odinga ambao tukiuchezea katika jumuia ya wapigakura, tutamrambisha sakafu hata kabla ya kura ya kwanza kupigwa,” akasema Nyoro.

Anasema kuwa Odinga hana ile mikiki ya mwisho ya kumalizia mchezo na “huwa tu anavuruga bahari iwe chafu na ngumu kuogelea humo kisiasa lakini wa kuibuka mshindi huwa ni mwingine jinsi historia ya uwaniaji wake inavyojitokeza.”

Anasema kuwa Odinga kwa sasa anawakilisha nembo ya kuwania akipoteze na hilo limewakosesha wafuasi wake wengi imani wakiona kuna nuhusi.

Ingawa Odinga hajatangaza waziwazi kuwa atawania urais 2022, akisisitiza kuwa atatoa mwelekeo wake baada ya mpango wa maridhiano BBI kuidhinishwa, kuna mengi ya kuwafanya wachanganuzi kuamini kuwa atawania.

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe tayari ametangaza kuwa taifa linafaa lijiandae kwa urais wa Bw Odinga 2022.

Murathe huchukuliwa kama kipaza sauti cha mawazo ya Rais Uhuru Kenyatta na katika siku za hivi karibuni ameonekana akipanga njama ya 2022 katika boma la Katibu Mkuu wa Cotu Francis Atwoli lililo katika Kaunti ya Kajiado.

Murathe, Odinga, aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth na Seneta wa Siaya James Orengo wameonekana sio mara moja katika boma hilo na kisha kutoa picha zao wakionekana kuwa katika ile hali ya urafiki wa chanda na pete na hivyo basi kujiangazia kama mrengo unaosukwa wa uwaniaji wa 2022.

Katika hali hiyo, Murathe akiibuka hadharani na kutangaza kuwa taifa lijiandae kwa urais wa Bw Odinga sio suala la kuchukuliwa kwa wepesi.

“Hatuchukulii kwa wepesi bali tunashabikia hilo kimyakimya kwa kuwa wapinzani wetu wanajiweka katika mtego wetu wa kuwavuta hadi kwa maangamizi ndani ya debe,” akasema Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua.

Aliyekuwa mbunge wa Maragua Elias Mbau anasema kuwa Odinga “atawania kama mradi wa serikali ya Jubilee na kwamba mrengo wa Rais na mrengo wa Jubilee wa Dkt Ruto wote wana uhuru kumenmyana iibuke nani mkali kati ya wao wawili.”

Anasema kuwa ni suala lililosukwa na kuandaliwa mezani kama mrengo wa uwaniaji 2022 ambapo Kenneth ndiye atashirikiana na Odinga kama ‘tiketi ya uwaniaji ya handisheki’.

“Ukitaka kujua maneno yangu ni halali na yaliyojaa ukweli, kwanza ujue kwamba kwa kila maneno 10 ambayo Murathe huongea kuhusu serikali ya sasa na urithi wayo baada ya kura ya 2022 ujue kwamba maneno tisa ni ya Rais na moja tu ndilo la Murathe. Ametangaza ni Odinga kumaanisha asilimia 90 ya tangazo hilo ni la Rais mwenyewe,” akaambia Taifa Leo.

Tayari, mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi ametangaza kuunga mkono uwaniaji wa Odinga na Kenneth akisema kuwa “ndio mrengo wa ushindi.”

Hata hivyo, wafuasi wa Dkt Ruto wakiwemo mbunge wa Kandara Alice Wahome, Seneta wa Nakuru Susan Kihika na mbunge wa Bahati Kimani wa Ngunjiri wanasema hiyo ni tiketi ya baraka kwa Dkt Ruto na wako tayari kumzamisha waziri mkuu huyo wa zamani.

Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungw’a anasisitiza kuwa “ikiwa kuna mtu rahisi wa kushinda 2022 ni Odinga na ni kwa sababu tele.”

Sababu hizo zinaanza kuchambuliwa na Bw Ngunjiri anayesisitiza kuwa Odinga kwa sasa yuko katika vita vikuu na wafuasi wake wa jadi aliowasaliti katika ‘kingo za mto Jordan akiwaelekeza Canaan’.

Anasema kuwa Odinga aliwahadaa katika kingo hizo eti kwanza wangojee avuke akashike doria ng’ambo ile nyingine ndio akiona ku salama awarejelee.

“Lakini alipovuka Mto Jordan na kuingia Canaan – ndani ya Jubilee – alikaribishwa kwa minofu na hela akawasahau wafuasi wake waliobaki ng’ambo ile ya mto na alipojitokeza aking’aa kiafya kutokana na mazuri, akawaambia watawanyike kama hali ya dharura kwa kuwa ‘huo mto umejaa mamba’,” asema Ngunjiri.

Anasema kuwa Odinga kujiosha nembo ya usaliti wa hali ya juu kuhusu hiyo safari ya Canaan haitakuwa kazi rahisi kwake na hivyo basi kuwa rahisi kumshinda kwa kura ya 2022.

Na ni kama dua yao inasikika kila kuchao kwa kuwa mshirika mkuu wa Bw Odinga akiwa ni Junet Mohammed tayari ametangaza kuwa “sisi kinara wetu huwa ni mmoja tu na anafahamika na kila mtu kwa hivyo hizi siasa za kubahatisha kuhusu hatima yetu ya 2022 zinafaa kukomeshwa.”

Hivi karibuni, kakake Odinga—Oburu Odinga—aliteleza ulimi na akatangaza kuwa “sasa mbele iko sawa kwa kuwa Odinga amepata ule uungwaji mkono wa wakwasi wa serikali ambao amekuwa akikosa katika uwaniaji wake hadi sasa hivyo basi 2022 utakuwa mteremko.”

Ingawa alizomewa kwa kumwaga mtama penye kuku wengi, ujumbe ulikuwa ushafika.

Mchanganuzi wa siasa za Mlima Kenya Prof Ngugi Njoroge anasema kuwa uwaniaji wa Dkt Ruto ili uibuke na ushindi kwa kiwango kikuu unahitaji apate ufuasi wa zaidi ya asilimia 80 eneo hilo.

“Huu ufuasi ndio upatikane, ni lazima mpinzani wake mkuu awe ni Bw Odinga kwa kuwa wapigakura wa eneo hili wakisikia jina la Odinga liko katika ushindani wa kuwa Rais, wao hujumuika pamoja kupinga. Katika kujumuika huko, hujitokeza sio kupigia Rais mfaafu zaidi kura bali kupinga Odinga asipite. Hapo ndipo afueni ya Ruto Mlima Kenya iko; wakipinga Odinga, yeye anufaike,” asema.