• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Baadhi ya wanaharakati hawaoni haja ya BBI na kura ya maamuzi kwa sasa

Baadhi ya wanaharakati hawaoni haja ya BBI na kura ya maamuzi kwa sasa

Na WINNIE ATIENO

BAADHI ya mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yamewapa changamoto Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga huku wakiwasihi kuzima azma yao ya kura ya maoni.

Sababu moja wanayoitoa ni kwamba taifa limeyumbishwa na janga la corona.

Wakiongea kwenye maadhimisho ya miaka 10 tangu urasmishaji wa katiba ya 2010, wamewataka Wakenya wawe makini na waupige msasa Mpango wa Maridhiano (BBI) unaoshabikiwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Tupinge BBI kwa hali na mali, inadhamiria kugawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila. Hii leo tukiadhimisha miaka 10 ya Katiba Mpya hatuna cha kufurahia kwani ni majonzi, ufukara na ukosefu wa ajira, wakenya wamekumbwa na baa la njaa, magonjwa huku ufujaji wa fedha ukiendelezwa,” alisema Bw Francis Auma mtetezi wa haki za kibinadamu kutoka shirika la Kiislamu la MUHURI.

Mtetezi wa Haki za Kibinadamu kutoka Muhuri Bw Francis Auma akihutubu akiwa mjini Mombasa, Agosti 27, 2020. Picha/ Winnie Atieno

Akiongea kwa niaba ya mashirika ya kutetea haki za kibinadamu nje ya shule ya msingi ya Star of the Sea mjini Mombasa, Bw Auma amewataka Wakenya washurutishe serikali kutekeleza Katiba hiyo.

“Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga wameanza mikakati ya kusema kura ya maamuzi yaja wakati umma hauoni haja nayo. Msiharibu Katiba,” amesema Bw Auma.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya Rais Kenyatta kutangaza uwezekano wa kura ya maamuzi; refarenda.

Kiongozi wa nchi alisema wakati mwafaka wa kutekeleza mabadiliko kwenye Katiba hiyo ni sasa.

Hata hivyo, watetezi hao wa haki za kibinadamu wanasisitiza kuwa juhudi za serikali kufanya mageuzi ya Katiba tangu Mwaka 1963 yamekuwa donda sugu na kuchangia utawala wa mkono wa chuma.

Kadhalika wamemshtumu Rais kwa ‘kuadhibu’ mahakama kwa kuwanyima fedha na ‘kukataa’ kuwaajiri majaji 41 walioteuliwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

Mkurugenzi mkuu wa mashirika ya kijamii ya kutetea haki za kibinadamu eneo la Pwani, Bw Zedekiah Adika amesifu Katiba hiyo akisema ilizalisha ugatuzi ambao umeleta maendeleo nchini.

You can share this post!

Omwenga azikwa

Sabina Chege apinga mpango wa elimu mashinani