• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:54 PM
Mwigizaji wa Amerika Chadwick Boseman afariki baada ya kuugua saratani

Mwigizaji wa Amerika Chadwick Boseman afariki baada ya kuugua saratani

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

MWIGIZAJI raia wa Amerika Chadwick Boseman anayefahamika kuigiza katika filamu inayojulikana kama ‘Black Panther’ amefariki baada ya kuugua saratani.

Boseman, 43, alifariki nyumbani kwake Los Angeles mbele ya mkewe na watu wa familia yake, kulingana na taarifa katika mtandao wa kijamii Ijumaa jioni. Ulikuwa unasalia mwezi mmoja tu aitimize umri wa miaka 44.

Msanii huyo alipatikana na saratani ya utumbo (colon cancer) miaka minne iliyopita, lakini hakutangaza matokeo hayo kwa umma.

Habari za kifo cha Boseman kimewashangaza wakereketwa katika sekta ya filamu ulimwenguni.

Jordan Peele ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kampuni ya filamu ya Get Out alisema kifo hicho ni “pigo kubwa kwa sekta ya filamu”.

“Alipambana kijasiri. Chadwick alivumilia changamoto nyingi, na akawaletea nyie mashabiki filamu nyingi ambazo mlipenda zaidi,” familia ya mwendazake ikasema kwenye taarifa.

Pia aliigiza katika filamu kama vile Marshall, Da 5 Bloods, August Wilson’s na zingine nyingi.

Filamu hizo zilitengenezwa wakati ambapo Boseman alikuwa akipokea matibabu.

Hata hivyo, anakumbukwa kutokana na uigizaji wake katika filamu maarufu, ‘Black Panther’ kuanzia mwaka wa 2018.

You can share this post!

Jobita ahakikishia mashabiki usimamizi kurejesha uthabiti...

Lazio wasajili ‘nyani’ mkongwe Pepe Reina