Habari Mseto

Dkt Ruto na Murathe waendelea kupapurana hadharani

August 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

 Na CHARLES WASONGA

MALUMBANO kati ya Naibu Rais William na Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe yaliendelea kutokota Jumamosi, Ruto akimtaka Murathe abanduke kutoka chama hicho.

Naibu huyo wa Rais alimkaripia Murathe akisema anawahujumu wanachama wa chama hicho tawala kwa kuunga mkono Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Dkt Ruto alisema hatua ya afisa huyo kuunga mkono mgombeaji urais kutoka chama kingine ni sawa na kuwahujumu wanachama wa Jubilee wanaokimezea mate kiti cha urais.

“Haina maana kwa maafisa wa chama kutangaza kuwa mwaniaji kutoka chama kingine ndiye atakuwa Rais. Ikiwa ni hivyo, basi waende jumba la Orange House washirikiane na watu hao kuendeleza ajenda hiyo,” akasema.

Dkt Ruto akaongeza: “Wale walioko jumba la Jubilee na wameamua kuunga mkono mgombeaji kutoka jumba la Orange wafunganye virago na waende. Wanafanya nini katika ofisi ya chama chetu?”.

Naibu Rais alisema hayo Jumamosi katika maeneobunge ya Nyali na Mvita, Kaunti ya Mombasa alipofanya msururu wa mikutano na viongozi wa kidini na kisiasa.

Kauli ya Dkt Ruto imejiri siku moja baada ya Bw Murathe kumtaka ajiondoe Jubilee ikiwa haridhiki na mabadiliko yaliyofanywa wiki kadhaa zilizopita katika usimamizi wa chama hicho tawala.

“Ruto alilenga kuteka chama na hivyo kuliendesha kama mali yake binafsi. Kile tulichofanya ni kuokoa chama na kukirejesha kwa wenyewe. Ikiwa alikerwa na hatua hiyo basi aondoke,” Bw Murathe akanukuliwa na gazeti la Saturday Nation akisema.

Akaongeza: “Mambo bado; hicho kilikuwa kionjo tu. Subiri tu; atajua hajui. Tutamthibitishia kuwa yeye sio mwerevu anavyodhani.”

Lakini Jumamosi Dkt Ruto alisema hatishwi na matamshi kutoka kwa matapeli wa kisiasa ambao wanataka kumzuia kuwania urais kwa tiketi ya Jubilee.

“Tuko tayari kwa kinyang’anyiro cha 2022 kwa misingi ya rekodi yetu ya maendeleo na sera ambazo zitaboresha nchi yetu kwa manufaa ya Wakenya wote,” akasema.

Aliandamana na wabunge; Mohamed Ali (Nyali), Benjamin Tayari (Kinango), Lydia Haika (Mbunge Mwakilishi, Taita Taveta), Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Wangui Ngirici (Mbunge Mwakilishi, Kirinyaga) Gladys Sholei (Mbunge Mwakilishi, Uasin Gishu) na Kimani Ichungwa (Kikuyu).