Ida Odinga azoa Sh200m katika harambee ya muda wa saa mbili
Na WAANDISHI WETU
AZMA ya Bi Ida Odinga, mkewe Kiongozi wa ODM Raila Odinga kujenga maktaba na kituo cha utafiti katika shule ya upili alikosomea, ilipigwa jeki alipofanikiwa kuchangisha takriban Sh200 milioni kwa karibu saa mbili pekee Ijumaa jioni.
Harambee huyo iliyoandaliwa katika hoteli ya Ole Sereni, Nairobi ilizoa mamilioni ya fedha kutoka kwa wanasiasa wakiwemo magavana, wabunge na maseneta.
Karibu viongozi wote wa kisiasa wa ODM walichangia, kando na viongozi wa vyama vingine akiwemo Rais Uhuru Kenyatta.
Rais Kenyatta alitoa mchango wa Sh6 milioni, naye nduguye, Bw George Muhoho akatoa Sh4 milioni.
Mama Ida, ambaye mapema wiki iliyopita aliadhimisha miaka 70 tangu kuzaliwa kwake, alipokea mchango kutoka kwa familia yake, marafiki na wadhamini huku akilenga kupata Sh300 milioni kufanikisha mradi huo.
Ujenzi wa maktaba na kituo cha utafiti unatarajiwa kufanywa katika Shule ya Upili ya Ogande, Kaunti ya Homa Bay ambapo alisoma zaidi ya miaka 50 iliyopita.
Kulingana na wadadisi, harambee hiyo iliyoanza mwendo wa saa kumi na nusu jioni ilitoa nafasi kwa wanasiasa, hasa walio wanachama wa ODM, kudhihirisha uaminifu wao kwa Bw Odinga.
Familia ya Bw Odinga ilitoa Sh16 milioni, naye Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko akitoa Sh3 milioni akaahidi kuongeza Sh2 milioni baadaye.
“Ida amekuwa nami wakati wote. Yeye ni mfano wa kuigwa. Ameteseka sana kwa ajili ya makosa yangu na nina deni kubwa la shukrani kwake,” Bw Odinga alisema katika hotuba yake.
Hazina ya Kitaifa ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) ya Homa Bay Mjini iliahidi kutoa Sh50 milioni, kupitia kwa Mbunge Peter Kaluma.
Makundi mbalimbali ya wabunge, wana na binti za Mama Ida, muungano wa wanafunzi wa zamani wa shule ya Ogande, marafiki wa Mama Ida na Wakenya wanaoishi ughaibuni, yalitoa takriban Sh100 milioni kwa jumla.
Magavana wengi waliokuwepo walitoa Sh1 milioni kila mmoja, isipokuwa Gavana wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana ambaye alitoa mchango wa Sh500,000.
Ripoti za Anthony Njagi, Justus Wanga na Walter Menya