Michezo

Arsenal yashinda Liverpool kwenye Community Shield kupitia penalti

August 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Pierre-Emerick Aubameyang alifunga penalti ya ushindi na kuwaongoza Arsenal kunyanyua ubingwa wa Community Shield baada ya kuwaangusha Liverpool 5-4 kwenye mechi iliyowakutanisha ugani Wembley, Uingereza mnamo Agosti 29, 2020.

Mshindi wa mechi hiyo aliamuliwa kupitia penalti baada ya pande zote kuambulia sare ya 1-1 mwishoni mwa muda wa dakika 90.

Arsenal ndio waliokuwa wa kwanza kuliona lango la Liverpool kupitia goli la Aubameyang kunako dakika ya 12 kabla ya chipukizi Takumi Minamino kusawazishia Liverpool katika dakika ya 73.

Bao la Minamino ambalo lilikuwa lake la kwanza kambini mwa Liverpool, lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na mshambuliaji matata mzawa wa Misri, Mohamed Salah.

Ingawa Arsenal walilalamikia refa kwamba bao hilo lilifumwa wavuni na Minamino baada ya Salah kunawa mpira, teknolojia ya VAR ilibainisha vinginevyo.

Huu ni mwaka wa pili mfululizo kwa Liverpool kupoteza ubingwa wa Community Shield kupitia penalti. Mwanzoni mwa msimu wa 2019-20, Liverpool walizidiwa maarifa na Manchester City kwa mikwaju 5-4 ya penalti uwanjani Wembley.

Aubameyang alidhihirisha umuhimu wake kambini mwa Arsenal ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha Mikel Arteta.

Nyota huyo mzawa wa Gabon alifunga tena mabao mawili mnamo Agosti 1, 2020 na kusaidia Arsenal kuwabwaga Chelsea 2-1 ugani Wembley. Ushindi huo wa Arsenal uliwanyanyulia ubingwa wa Kombe la FA msimu huu wa 2019-20.

Ushirikiano mkubwa kati ya Aubameyang, Bukayo Saka na Ainsley Maitland-Niles ulitatiza pakubwa mabeki wa Liverpool ambao walishuhudia safu yao ya ulinzi ikivuja kupitia chipukizi Neco Williams.

Na baada ya kila kikosi kupiga jumla ya penalty nne, Aubameyang aliendea mkwaju wa mwisho kwa upande wa Arsenal na kumzidi maarifa kipa matata wa Liverpool, Alisson Becker.

Aubameyang anajivunia kufungia Arsenal jumla ya mabao 71 kutokana na mechi 110 zilizopita, na hakuna mwanasoka yeyote katika historia ya Arsenal amewahi kufunga zaidi ya idadi ya magoli matano ambayo yamefungwa na Aubameyang uwanjani Wembley.

Mnamo Agosti 28, Arteta alikiri kwamba Aubameyang alikuwa pua na mdomo kutia saini mkataba mpya kambini mwa Arsenal.

Baada ya kutia kapuni mataji mawili chini ya kipindi cha mwezi mmoja, Arsenal watakuwa wamefunga rasmi kampeni za msimu huu ambao ni wa kwanza chini ya Arteta kwa matao ya juu zaidi iwapo Aubameyang atarefusha muda wa kuhudumu kwake ugani Emirates.

Ingawa Liverpool walikosa huduma za beki Trent Alexander-Arnold na kiungo Jordan Henderson, kocha Jurgen Klopp aliwajibisha kikosi ambacho kilikuwa na wanasoka waliokuwa na uwezo wa kuwapepeta Arsenal ambao pia walikosa maarifa ya mafowadi Nicolas Pepe na Alexandre Lacazette.