Siasa

JAMVI: Mfumo wa ugavi pesa za kaunti wageuka mtihani mgumu kwa Irungu Kang'ata

August 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na MWANGI MUIRURI

BAADA ya Rais Uhuru Kenyatta kuingiwa na wasiwasi kwamba ajenda za utawala wake zilikuwa zinakwamakwama katika bunge la kitaifa na lile la seneti, akiwa na wandani wake walizindua ‘msako’ mkali dhidi ya waasi katika mabunge hayo.

Matokeo yalikuwa kutimuliwa kwa wasimamizi (wengine wanasema wenyeviti) wa kamati mbalimbali na pia uongozi wa walio wengi.

Katika mchakato huo yule tunayemwangazia hapa – Seneta wa Kaunti ya Murang’a Irungu Kang’ata – alichukua nafasi ya kiranja wa wengi katika bunge la seneti.

Kang’ata alionekana na wandani wa Rais kama aliyekuwa na uwezo wa kusukuma ajenda za Jubilee ndani ya bunge hilo la seneti. Seneta wa Nakuru Susan Kihika alitimuliwa ndipo Kang’ata akapata nafasi ya kupaa kutoka unaibu.

Kazi za mwanzo katika majukumu yake mapya zilikuwa ni kusukuma kuondolewa kwa waasi hasa waliohusishwa na ufiuasi kwa Naibu Rais Dkt William Ruto na pia kutoa mialiko ya vikao vya kinidhamu kwa maseneta wa Jubilee waliosusia mikutano ya kupanga njama za timuatimua hizo.

Kazi ikaonekana kuwa rahisi kwa Kang’ata na ambapo nyota yake ilitarajiwa kung’aa hata zaidi ikiibuka kuwa yeye ni mwenye bahati ya mtende maishani ambapo amekuwa akipanda ngazi ya mamlaka kwa haraka.

Alianza kama mwanaharakati katika siasa za Chuo Kikuu cha Nairobi akiwa kiongozi wa wanafunzi, akachaguliwa kuwa diwani Murang’a kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Kiharu na sasa ndiye Seneta wa Murang’a.

Kwa sasa anatazamiwa kuwania ugavana wa Murang’a 2022 hivyo basi kuhitaji matokeo ya ufanisi katika miradi yake ya sasa kisiasa ndipo ajiangazie kama mchapakazi wa kuleta matokeo na wala sio tu wa kupiga domo.

Mtihani rahisi kwa Kang’ata ulifika kikomo wakati alijipata kwa mtihani halisi wa cheo chake kipya cha kiranja wa wengi na ambao kuupita hata baada ya kuufanya mara 10 sasa huenda ikawa ni ndoto ya mchana.

Mtihani huo ni ule wa kuhakikishia Rais kuwa mfumo uliofadhiliwa na serilali ya Jubilee – wa ugavi wa pesa kwa serikali za kaunti ukizingatia idadi ya watu – unapitishwa ili utumike kwa miaka mitano ijayo.

“Huu sio mtihani tu, bali ni suala la kufa kupona kwa siasa za Kang’ata kwa kuwa akiupita, basi nyota yake ndani ya Jubilee itang’aa zaidi na pia eneo la Mlima Kenya ambalo limekuwa likitengwa na mfumo uliokuwa unatumika wa kugawa pesa kwa kutumia tathmini ya upana wa maeneo,” asema mchanganuzi wa siasa za Mlima Kenya Prof Ngugi Njoroge.

Anafafanua: “Kupandishwa hadhi hadi kuwa kiranja wa wengi seneti hakukumjenga Bw Kang’ata kwa kuwa alionekana kuwa msaliti wa imani kwa Dkt Ruto ambaye kwa sasa ndiye anawika Mlima Kenya.”

Anasema kuwa wafuasi wa Dkt Ruto Mlima Kenya hadi sasa hawajaonekana kung’atuka na kuhamia hadi kwa ari ya Rais Kenyatta na wandani wake wanaoonekana kupendelea urais umwendee mwingine kando na Naibu huyo wa Rais.

“Wanaofuatilia mitandao ya kijamii na pia mahojiano na vituo vya redio na runinga vinavyotangaza kwa lugha ya Gikuyu watakuambia kuwa Bw Kang’ata alifananishwa na Judas Iscariot ambaye ndiye alimsaliti Yesu Kristo akasulubiwe, Kang’ata akionekana kucheza nafasi hiyo ya kutumika kumsulubu Dkt Ruto,” asema.

Lakini sasa Kang’ata ana nafasi ya kujinasua kutoka nembo hiyo ikiwa ataonekana kujituma na afaulu kupisha mfumo huo katika bunge la Seneti na ambao hadi sasa unaonekana kupingwa kwa dhati.

“Kwa mara kumi sasa Kang’ata ameonekana kutokuwa na mbinu ya kushawishi kupitisha kwa mfumo huo. Ameonekana kukosa mkakati wa ushawishi na mara kwa mara ameonekana kurejelea madai yasiyo na ushahidi, vitisho na malalamiko yasiyo na mwelekeo,” asema mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua.

Kang’ata amesikika akitisha kiongozi wa ODM Raila Odinga kuwa ikiwa hutashurutisha maseneta wa mrengo wake kupitisha mfumo huu wa serikali, “basi sisi ndani ya Jubilee tutahakikisha kuwa hatuungi mkono Handisheki na pia mpango wa maridhiano ya kitaifa wa BBI.”

Hatimaye, Rais Kenyatta, madai yapo kuwa binafsi alimpigia simu Kang’ata akimuonya dhidi ya kutumia BBI na Handisheki kiholela.

Siku chache baadaye Kang’ata akaandaa mlo wa mchana kwa maseneta dhamira yake ikiwa ni kuwavuta wapitishe mfumo huo lakini Ikulu ikasemwa kufutilia mbali dhifa hiyo na kumwacha Kang’ata akiwa na mapochopocho yasiyo na matumbo ya kufaidi.

Hivi karibuni, Kang’ata amesikika akidai kuwa kuna magavana ambao wanawahonga baadhi ya maseneta wasipitishe mfumo wa serikali na pia kuwa Dkt Ruto pia ni msaliti wa serikali kupitia kutojituma kwake moja kwa moja kuwaongoza maseneta wa mrengo wake kuunga mkono.

Aidha, ametisha kushtaki waandishi wa habari wa Murang’a ambao watamnukuu akiongea kwa lugha ya Gikuyu “kwa kuwa nikiongea kwa lugha ya mama huwa naongea kuhusu mambo ya nyumbani lakini ukitaka kuninukuu subiri mpaka niongee Kiingereza au Kiswahili na tuelewane namna utakavyoandika.”

Hii ni baada ya kunukuliwa kuhusu madai ya magavana kuhonga maseneta ili mfumo huo usipitishwe.

Aliyekuwa mbunge wa Maragua Elias Mbau na ambaye ni mshirika wa karibu wa aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth anafichua kuwa mambo ni magumu kwa Kang’ata kiasi kwamba “tunamsaidia kusaka mbinu ili mfumo huo upitishwe.”

Anafichua kuwa Bw Kenneth ambaye anaonekana kama anayeandaliwa na Rais Kenyatta kuchukua majukumu ya msemaji wa jamii za Mlima Kenya ameungana na Naibu mwenyekiti matata wa Jubilee David Murathe kupiga jeki juhudi za Kang’ata.

“Umewaona hao wakiungana na Bw Odinga pamoja na Seneta wa Siaya aliye kinara wa walio wachache Seneti James Orengo, Katibu mkuu wa muungano wa wafanyakazi nchini (Cotu-K) Bw Francis Atwoli na wengine kusaka suluhu la mfumo huo,” akasema.

Alisema kuwa kuundwa kwa kamati maalum ya maseneta 12 kusaka suluhu la kupitishwa kwa mfumo wa kugawa pesa hizo ni mojawapo ya jitihada za mradi wa kumwokoa Kang’ata.

Huku bunge la Seneti likitarajiwa kuandaa kikao kingine karibuni kusaka suluhu hili, kwa Kang’ata ni roho mkononi ikizingatiwa kuwa Kaunti hazina ufadhili kwa miezi mitatu sasa mfululizo, hali ambayo imesababisha kuwepo kwa minong’ono na migomo ya wafayakazi huku huduma zikizidi kukwama, hali ambayo sio ya kumjenga Bw Kang’ata bali ni ya kumbomoa.

Katika haya masaibu, Kang’ata anasisitiza kuwa atapita mtihani huu na hatimaye aibuke thabiti zaidi.

“Hata ikiwa hili ni suala la uwajibikaji wa Seneta kama kiongozi binafsi anayetazamiwa atoe suluhu la haki ya ugavi raslimali, mimi nikiwa tayari mimetoa msimamo wangu kwa niaba ya watu wa Murang’a, hatimaye nitawajibikia majukumu yangu kama mshirikishi wa ajenda ya serikali na nina uhakika nitatoboa,” akasema Kang’ata.