Michezo

Beki Keane atia saini mkataba mpya na Everton hadi 2025

August 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

BEKI matata wa Everton, Michael Keane ametia saini mkataba mpya wa miaka mitano ambao kwa sasa utamdumisha ugani Goodison Park hadi Juni 2025.

Keane, 27, alijumuishwa na kocha Gareth Southgate katika timu ya taifa ya Uingereza mnamo Agosti 25, 2020 ambayo kwa sasa inajiandaa kupambana na Iceland na Denmark mwezi ujao kwenye michuano ya Uefa Nations League.

Hadi kufikia sasa, Keane amewajibishwa na Everton mara 94 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) tangu ajiunge na kikosi hicho kutoka Burnley mnamo 2017.

Kwa kurefusha muda wa kuhudumu kwake kambini mwa Everton, Keane amezima tetesi zilizokuwa zikimhusisha na uwezekano wa kujiunga na Manchester United, Bayern Munich, Borussia Dortmund, Atletico Madrid na AS Roma.

“Natazamia kujivunia misimu ya kuridhisha zaidi kambini mwa Everton. Miaka mitatu iliyopita ugani Goodison Park imekuwa ya mafanikio tele. Nalenga kujibidiisha zaidi muhula ujao na kuridhisha mashabiki na waajiri wangu,” akasema sogora huyo.

Everton wanajivunia ufufuo mkubwa chini ya kocha Carlo Ancelotti aliyepokezwa mikoba ya kikosi hicho mnamo Disemba 2019. Katika msimu wake wa kwanza ugani Goodison Park, Ancelotti aliongoza Everton kutinga nafasi ya 12 kwenye msimamo wa jedwali la EPL mnamo 2019-20.