• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Wajane wazee walia kubakwa na vijana usiku

Wajane wazee walia kubakwa na vijana usiku

ERIC MATARA na PHYLLIS MUSASIA

HOFU imetanda katika eneo la Dundori, Nakuru kufuatia ongezeko la visa ambapo wanawake wajane hushambuliwa na kubakwa usiku na wanaume wasiojulikana.

Taifa Leo ilihesabu wanawake 16 ambao walisema walibakwa katika muda wa miezi mitatu iliyopita, wengi wao wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 60.

Kati yao, ni nyanya mwenye umri wa miaka 90 ambaye aliripotiwa kubakwa mara tano, kila wakati mvua ilikuwa ikinyesha.

Viongozi wa nyumba kumi pamoja na wakazi wa eneo hilo waliwaonyoshea kidole cha lawama vijana wa eneo hilo ambao wanatumia dawa za kulevya na kubugia pombe kiholela.

“Hatuna maafisa wa polisi eneo hili ambao hushika doria, haswa nyakati za usiku wanapohitajika. Wahalifu wanapata muda wa kutosha kuhanganisha wakazi usiku na mchana,” akasema mzee mmoja wa nyumba kumi.

Vijiji vilivyoathirika zaidi ni pamoja na Juakali, Kaburini na Tia Wera. Mnamo Julai 5, mwendo wa saa tatu usiku, mjane mwenye umri wa miaka 60 alibakwa na mwanamume aliyemvamia nyumbani kwake.

Kulingana na mwathiriwa, hakumtambua mtu huyo kwani alimshika kwa nguvu katika giza alipotoka nje kuangalia ng’ombe wake zizini.

“Giza lilitanda na kitendo hicho kilifanyika kwa haraka. Sikumjua huyo mwanamume lakini kulingana na jinsi alivyonishika na kunilaza sakafuni, alikuwa mrefu,” akasema.

Mama huyo wa watoto watano alisema kuwa tangu wakati huo ameishi akihofia kwamba huenda akabakwa tena.

Katika kijijji jirani, mjane wa umri wa miaka 62 alisema pia yeye anaishi kwa uoga baada ya kutendewa unyama huo.

“Nilishambuliwa nyumbani kwangu na wanaume watatu ambao walinibaka mbele ya wajukuu wangu. Mwendo wa saa mbili usiku, watu hao walinishika na kunifunga na kamba kabla ya kunibaka mmoja baada ya mwingine,” akasema.

Alisema kuwa aliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha eneo hilo lakini hajapata kusaidika.

Msaidizi wa Kamishna wa Kaunti anayesimamia eneo la Dundori, Bw Henry Kirwa alisema alikuwa na taarifa kwamba visa hivyo vimeenea, ila waathiriwa wengi huwa hawapigi ripoti rasmi kwa polisi.

You can share this post!

Kanisa Katoliki lapinga refarenda ya kujali wachache

Wiper yaishtaki ODM kuhusu uongozi bungeni