Siasa

Ruto aongoza wimbo akirejea kanisani kwa kishindo

August 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto Jumapili alirejea kanisani kwa kishindo, baada ya karibu miezi sita tangu virusi vya corona vilipotangazwa kufika nchini mnamo Machi.

Dkt Ruto alishiriki kwenye ibada katika kanisa la AIC Pipeline, eneobunge la Embakasi Kusini, Kaunti ya Nairobi ambako hata alipata nafasi kuongoza wimbo baada ya kueleza furaha yake kuhusu kurejelewa kwa ibada kanisani.

Hotuba yake iliashiria atatumia nafasi hii sasa kuvumisha msimamo wake kuhusu marekebisho ya katiba kwa waumini, huku akiendelea kutoa ahadi za maendeleo na kuahidi kusaidia kukamilisha miradi ya makanisa.

“Ni lazima viongozi wafahamu kwamba Wakenya wengi kwa sasa wanapitia hali ngumu kutokana na janga la virusi vya corona. Hivyo, lazima wayape kipao mbele maslahi ya wananchi badala ya kujijali pekee,” akasema Dkt Ruto.

Tangu serikali ilipozima ibada makanisani kwa ajili ya kuepusha maambukizi ya virusi vya corona, Dkt Ruto alikuwa akishiriki ibada na familia yake katika makazi yake, mtaani Karen jijini Nairobi.

Vile vile, alikuwa akishiriki ibada na viongozi mbalimbali wa kidini kutoka sehemu tofauti nchini ambao wamekuwa wakimtembelea.

Dkt Ruto amekuwa akitumia makanisa kama jukwaa kuu kujijenga kisiasa na kuwashambulia washindani wake, hasa kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kwa madai ya “kuvuruga” Chama cha Jubilee (JP) kupitia handisheki kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.

Jana, alieleza imani kwamba hali ya kawaida itarejea, hasa baada ya serikali kuruhusu ibada makanisani kuendelea kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa za kudhibiti maambukizi.

“Tunatarajia kwamba hali ya kawaida itarejea, hasa baada ya visa vya maambukizi kuanza kupungua,” akasema.