• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Rais akiri corona ilimchanganya sana

Rais akiri corona ilimchanganya sana

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta amefungua roho kuhusu mahangaiko ambayo amekuwa akipitia tangu janga la corona lilipoingia nchini mnamo Machi.

Katika hotuba yake jana alipofungua rasmi kongamano kuhusu ugonjwa wa Covid-19 ambalo liliandaliwa na Baraza la Magavana kupitia kwa mtandao wa video, Rais alikiri hali haijakuwa rahisi kwake kama kiongozi wa taifa kutoa maamuzi muhimu katika kipindi hiki.

Tatizo kubwa ambalo humwandama ni kuhusu kuamua kama jambo la muhimu ni kulinda maisha ya raia kwa kuweka kanuni kali za kuepusha ueneaji virusi vya corona, au kulinda uchumi na riziki ya raia, ambayo inaweza kutoa mwanya wa ueneaji maambukizi.

“Nimekuwa nikipitia mtanziko wa mawazo kufanya maamuzi. Ilikuwa vigumu sana kufanya maamuzi kati ya mambo mawili ambayo yote ni ya haki. Hakujawahi kuwa na wakati wowote katika taifa hili ambapo rais ametakiwa kutoa kanuni zinazozuia watu kufurahia uhuru wao,” akaeleza.

Tangu wakati kisa cha kwanza cha ugonjwa wa Covid-19 kilipotangazwa nchini, wananchi wamepitia hali ngumu kutokana na kanuni kali kama vile kafyu, kufungwa kwa baadhi ya miji na mitaa, amri za kutotangamana miongoni mwa kanuni nyinginezo.

Alikiri pia kuwa kanuni hizo kali zimesababisha matatizo mengi katika jamii hasa vijana wanaokumbwa na msongo wa mawazo.

“Ninaagiza Wizara ya Afya itambue jinsi tutakavyotatua tatizo la msongo wa mawazo unaokumba wananchi hasa vijana wetu,” akasema.

Hata hivyo, Rais Kenyatta alisema ni kutokana na masharti hayo ambapo sasa idadi ya wagonjwa wanaotangazwa kila siku imeanza kupungua.

Licha ya mwelekeo huo wa idadi kupungua, alirai wananchi wasianze kuzembea katika kudumisha kanuni za kuepusha maambukizi hadi wakati kutakapokuwa na thibitisho kamili kwamba nchi imepata ushindi dhidi ya virusi vya corona.

“Habari njema ni kwamba idadi imeanza kupungua, lakini tusianze kusherehekea mapema. Hii ni kwa sababu imethibitishwa idadi huanza kupungua baada ya kufika kileleni. Huu ni wakati hatari kwani kutoka hapa, idadi inaweza kuanza kupanda tena,” akasema.

Kongamano hilo lililokuwa wazi kwa umma lilihudhuriwa pia na magavana wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Bw Wycliffe Oparanya, na mawaziri akiwemo Mutahi Kagwe (Afya), Eugene Wamalwa (Ugatuzi) na Betty Maina (Biashara).

Mabalozi kadha na wawakilishi wa mashirika ya kutetea haki za binadamu pia walikuwepo.

Kongamano hilo lilinuiwa kufanya utathmini wa hatua ambazo Kenya imepiga kufikia sasa, na kutoa mwelekeo kuhusu hatua zinazofaa kuchukuliwa kwenda mbele. Ilinuiwa pia kutambua hatua zinazofaa kuchukuliwa katika miaka ijayo endapo kutatokea janga lingine la aina hii.

Miongoni mwa changamoto ambazo zilitambuliwa ni kama vile ufisadi katika ununuzi wa vifaa muhimu vya kupambana na Covid-19, ukatili wa polisi wanaposimamia umma kutekeleza kanuni, serikali kuu kuchelewa kutoa fedha kwa serikali za kaunti, na kaunti nyingi kukosa uwezo wa kutoa matibabu ya dharura.

Kwa upande mwingine, mafanikio mbalimbali yalitambuliwa kama vile ubunifu wa hali ya juu wa Wakenya kujitengenezea vifaa muhimu vya kimatibabu.

You can share this post!

Kesi zaumiza raia

Uhuru aagiza KEMSA ianike tenda zote mtandaoni