• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
GWIJI WA WIKI: Nyota ya Almasi yazidi kung’aa

GWIJI WA WIKI: Nyota ya Almasi yazidi kung’aa

Na CHRIS ADUNGO

ALMASI Ndangili ni miongoni mwa vijana wachache wa kupigiwa mfano kutokana na mafanikio yao kitaaluma na jinsi wanavyotumikisha talanta na vipaji walivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu.

Nyota ya Almasi ambaye kwa sasa anasomea shahada ya uzamili katika masuala ya biashara katika Chuo Kikuu cha USIU-Africa, inazidi kung’aa kupitia upekee wa ubunifu wake.

Itakumbukwa kwamba Almasi hajasomea Kiswahili katika Chuo Kikuu kwani shahada yake ya kwanza ni ya kompuyta ya sayansi na amekuwa akijishughulisha na masuala ya teknolojia kwa takriban miaka kumi sasa.

Almasi anaamini kuwa si lazima usome kamusi nzima ya Kiswahili kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho ndipo ukifahamu Kiswahili.

“Sawa na lugha yoyote nyingine, Kiswahili ni chombo tu tunachotumia kuwasilisha sera na mawazo yetu. Zaidi ya hapo, kufanikiwa kwako kutategemea jinsi utakavyojenga urafiki na watu na kudumisha mlahaka mwema.”

“Jiulize namna unavyotumia ubunifu wako kuendesha shughuli zako za sanaa, hasa katika uandishi wa Kiswahili. Jiulize jinsi utakavyoongeza thamani kwa wanaofuatilia kazi zako. Hiyo ndiyo njia bora kabisa ya kupima mafanikio yako,” anasema.

UANDISHI, TAMASHA YA KISWAHILI

Katika umri wa miaka 19, Almasi alichapisha kitabu chake cha kwanza ‘Chozi La Ukweli Mchungu’. Kupitia tamthilia hii, anatumia ubunifu wake kusuka kisa cha mhusika Kamjesh anayezaliwa kijijini Buzeki na kujipata bila mama mzazi. Hakujua hili hadi alipotimu umri wa kubaleghe kisha baba na mama mlezi wakampasulia mbarika kwamba baada ya kuzaliwa kwake, alitupwa katika jaa la taka.

Kwa kuwa damu ni nzito kuliko maji, mtoto wa maskini anaamua kuchomoka kijijini Buzeki kuelekea Singisingi alikompata mamaye akiwa mwendawazimu. Zaidi ya uandishi wa vitabu anakozidi kutopea, Almasi ametunga zaidi ya michezo 200 ya kuigiza kwa Kiswahili na Kiingireza.

“Mimi ni mwanasayansi kitaaluma na ninaamini hakuna watu wazuri zaidi katika utunzi kuliko wanasayansi. Sayansi huhitaji ubunifu wa hali ya juu zaidi na ina maana kuwa endapo umebobea katika masuala ya sayansi na teknolojia, kuna uwezekano uwe mwandishi wa kazi za kuvutia hata zaidi. Endapo unaamini kwamba una uwezo wa kuyazamia mambo mawili kwa wakati mmoja na ufanikiwe, mbona ulifanye moja?”

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kujenga upya taswira ya Kiswahili miongoni mwa vijana wanaojichipukia katika taaluma mbalimbali. Almasi anaamini kwamba kila mpenzi wa Kiswahili anastahili kujihisi kuwa ana nafasi katika jamii pana ya Waswahili bila ya kuonekana kuwa ‘mpinzani’.

Kupitia Tamasha ya Kiswahili ambayo ni zao la mawazo ya Almasi, ushirikiano imara kati ya washikadau wa Kiswahili wakiwemo wachapishaji, vyombo vya habari, mashirika ya serikali, kampuni mbalimbali na watu binafsi, umewapa vijana wengi majukwaa ya kutambua vipaji vyao katika sanaa za ushairi, uigizaji na utambaji wa hadithi jukwaani.

“Tumeona matunda na ukubwa wa taathira ya tamasha hizi ambazo hutoa jukwaa kwa wapenzi wa Kiswahili kuhimizana, kubadilishana mawazo na kuburudishwa na Kiswahili.”

Japo anahisi kwamba bado hajafanya mengi katika ulingo wa Kiswahili, Almasi anatambua na kujivunia ukubwa wa mchango wa Dkt Hamisi Babusa, Swaleh Mdoe, marehemu Prof Ken Walibora, Prof Kineene Wa Mutiso, Pauline Kea Kyovi, Kinyanjui Kombani, Prof Clara Momanyi na Munene Nyagah katika maadhimisho ya tamasha za awali.

“Hii inanipa imani kwamba ninachokifanya ni sahihi. Inanichochea kuwa mbunifu zaidi maana wapo maelfu ya vijana wanaotazamia kufaidika kutokana na hatua zangu.”

‘Kiswahili na Utamaduni’, ‘Kiswahili na Teknolojia’ na ‘Kiswahili na Talanta’ ni baadhi ya michezo iliyoandikwa na Almasi na kuwahi kuigizwa katika hafla za Tamasha ya Kiswahili chini ya udhamini wa KNLS, KICD, Oxford, Longhorn na Blaze (Safaricom).

“Hizi ni mada ambazo tumetumia kwa miaka iliyopita kukishabikia Kiswahili,” anasema Almasi.

Almasi pia ni mwasisi na Meneja Mkurugenzi wa kampuni ya Imarisha East Africa Productions Limited. Hii ni kampuni ambayo mnamo 2019, iliorodheshwa miongoni mwa bora zaidi duniani. Kutokana na hilo, Almasi alialikwa kuhudhuria mafunzo ya wiki mbili kuhusu masuala ya uendeshaji biashara katika eneo la Silicon Valley, Amerika.

“Huu ni utambuzi na hatua iliyonipa msukumo mkubwa. Ilikuwa fahari na tija kuona mtu wa mbali sana na niliko akijivunia ninachokifanya hapa nyumbani.”

UTABIRI WA HALI YA KISWAHILI KATIKA KARNE YA 21

Almasi anahoji kwamba merikebu ya Kiswahili inahitaji kujengwa upya katika Karne ya 21, na itajengwa upya na vijana kwa nguvu za ushawishi wala si majeshi, silaha au vifua.

Unaona Kiswahili kikikuwa wapi katika kipindi cha miaka kumi ijayo?

Kiswahili kitainuka na kupanuka sana kimatumizi katika mawanda mbalimbali kwa kuwa vijana wametambua thamani ya lugha hii na wana ari ya kueleza hadithi za Kiafrika kwa kutumia lugha yao. Sioni atakayekuwa na uwezo wa kupingana na hizi nguvu mpya.

Pili, ubunifu wa vijana wa zama hizi umekuwa wa hali ya juu ukilinganisha na zama za kale. Teknolojia na utandawazi imerahisisha mambo. Kumekucha na vijana wamechukuwa nafasi yao katika medani ya Kiswahili.

Tatu, lugha asili (za mama) zinafifia na lugha ya pili ambayo itatumiwa kwa urahisi kujieleza itakuwa Kiswahili. Tusidanganyike, Kiingireza hapa Kenya hakitumiki sana kuliko Kiswahili isipokuwa katika shughuli rasmi za kazi. Jiulize mbona wanasiasa hatupa Kiingereza na kuzamia Kiswahili wanapoomba kura za wananchi!

Unafikiri ni mbinu gani tunahitaji kutumia katika Karne ya 21 ili kukipa Kiswahili sura mpya?

Tuangazie Kiswahili katika mkondo wa sanaa na biashara. Tupanue fikra na tuone namna tutakavyoridhisha watu wengi tukiandika michezo ya televisheni au ya kuigizwa majukwaani. Tuwasilishe ujumbe kwa Kiswahili mufti bila kuteleza katika matamshi au matumizi ya ngeli.

Tukusudie kutumia mbinu mbalimbali za lugha na sanaa ya uandishi ili turutubishe kazi zetu. Tukomeshe tabia za kikale za kubishana kuhusu nani aliyebuni ngeli gani au nani bingwa wa mabingwa. Tupanie kuongozwa na falsafa hii ya marehemu Prof Ken Walibora: Tusigombanie fito, twajenga nyumba moja!

Kiswahili kinapitia changamoto zipi katika Karne ya 21?

Wapo wataalamu ambao bado wamezamia ukale. Kila mara ni kuwakosoa vijana na kuwavunja moyo. Hawafanyi hivi kwa kuwa vijana wanakosea, lakini kwa kuwa wanaogopa ushindani wa nguvu mpya. Tutiane moyo badala ya kutawaliwa na ubinafsi.

Je, Kiswahili kitalipa vipi katika karne hii ambapo vijana wengi wameonekana kuvutiwa na tamaduni za Kimagharibi?

Faidi ya Kiswahili itaonekana kupitia ubunifu wako. Tujifunze Kiswahili na kukitumia kitaratibu kueneza talanta zetu na kufanya biashara mbalimbali. Kazi za Kiswahili ni nyingi iwapo tutaanza kuibidhaaisha lugha hii. Lakini kumbuka, mtu huuza anachokielewa. Jaribu ukielewe Kiswahili.

Tueleze machache kuhusu Imarisha East Africa Productions.

Imarisha East Africa Productions ni kampuni ya kulea talanta miongoni mwa vijana wenye ari ya kukuza sanaa ya Kiafrika. Lengo ni kujenga sura mpya ya sanaa ambayo kwa kiasi kikubwa itaendeshwa na Kiswahili katika Karne ya 21.

Azimio letu litabakia kusaidiana na kampuni na mashirika ya elimu kunufaisha walengwa kwa kufyatua kazi za Kiafrika zitakazozingatia ubunifu wa vijana wetu na kutumia teknolojia kurahisisha namna ya kuwafikia wengi katika bara zima la Afrika. Tunaendesha miradi mbalimbali kama vile Tamasha ya Kiswahili ambapo tunapigia chapuo Kiswahili kupitia maigizo, tafsiri na programu anuwai zinazokuza talanta.

You can share this post!

Uhuru aagiza KEMSA ianike tenda zote mtandaoni

ANA KWA ANA: ‘Baiskeli ina faida tele kipindi hiki...