Wakazi wapinga ubomozi wa msikiti
Na MISHI GONGO
MZOZO ulizuka kati ya wakazi wa eneo la Kadzandani, eneobunge la Nyali, Kaunti ya Mombasa na maafisa wa serikali ambao walitishia kuvunja jengo la msikiti ili kutoa nafasi kwa ujenzi wa afisi ya serikali.
Kwa mujibu wa diwani wa wadi hiyo, Bw Francis Kombe Nzai, jana asubuhi naibu kamishna, Bw Henry Kemoi akiandamana na chifu wa eneo hilo walifika sehemu hiyo wakitaka kubomoa jengo hilo.
Anasema naibu kamishna huyo alidai kuwa sehemu hiyo ilipangiwa kujengwa afisi ya mwakilishi wa serikali.
Bw Nzai alisema ardhi hiyo ilikuwa imepangiwa kujengwa shule ya chekechea lakini kutokana na udogo wake, ujenzi wa shule hiyo ulipelekwa sehemu nyingine.
“Ardhi hii ni ya umma, iko katika skimu ya Mwache ya mwaka 1992. Madhumuni ya sehemu hii ilikuwa ni kujenga shule ya chekechea lakini kufuatia udogo wake ujenzi haukufanyika. Baadaye tuliambiwa tupendekeze mradi tunaotaka ufanywe sehemu hii kwa manufaa ya umma ndiposa tukaamua kujengwe msikiti,” akasema mwakilishi huyo.
Alisema ujenzi wa msikiti huo ulianza mwanzoni mwa mwaka lakini baada ya kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19, ujenzi ulisitishwa kwa muda.
“Tuliletewa wadhamini na gavana wetu Hassan Joho na tukawaonyesha eneo hili, hakuna aliyepinga ujenzi. Sasa tunashangaa serikali imejitokeza kutaka kufanya ubomozi baada ya ujenzi kuanza,” akasema.
Alidai kuwa naibu kamishna huyo aliagiza kusitishwa kwa ujenzi huo hadi pale watakapojadiliana na kamishna wa Mombasa Bw Gilbert Kitiyo.
Juhudi zetu kutafuta maoni kuhusu mzozo huo kutoka kwa Bw Kitiyo hazikufua dafu kwani hakupokea simu wala kujibu ujumbe aliotumiwa.
Mwenyekiti anayesimamia ujenzi wa msikiti huo Bw Adam Wario alisema si haki kwa serikali kusitisha ujenzi huo ambao utakuwa na manufaa kwa wakazi hao.
Aidha, aliomba serikali itafute sehemu nyingine kutekeleza ujenzi wao.“Ardhi hii ilikuwa imekaa bila shughuli yoyote kwa muda mrefu.
Kujengwa kwa msikiti hapa kutawasaidia wakazi kupata mafunzo ya dini na kuepusha vijana na maovu” akasema.
Mkazi mmoja Bi Saada Guyo alisema ujenzi huo wa msikiti na madrassa utasaidia kuwalinda watoto.
Alisema kwa sasa watoto wanalazimika kutembea mwendo mrefu kutafuta elimu jambo ambalo linachangia baadhi yao kubakwa au kupata ajali.
“Madrassa yanapatikana Bamburi. Tunalazimika kuwasafirisha watoto wetu kwa bodaboda au tuk tuk. Baadhi ya wahudumu huishia kuwanbaka na kuwalawiti watoto wetu,” akasema.
Aidha, alisema uwepo wa madrassa katika eneo hilo utawasaidia vijana kupata masomo ya kidini na kuwaepusha kushawishiwa kujiunga na makundi ya kigaidi kwa kukosa elimu.