Bima ya afya bado ghali kwa Wakenya, lakini suluhu zipo
Na SAMMY WAWERU
Kulingana na Wizara ya Afya takriban asilimia 13 ya Wakenya hawana uwezo kupata huduma za afya kwa sababu ya ukosefu wa fedha, huku asilimia 6 wakiwa katika hatari inayotokana na gharama ya ghafla ya matibabu wanapougua.
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Mpango wa Afya kwa Wote (UHC), asilimia 62 ya Wakenya hawana bima ya afya, bima ya NHIF ikiwakilisha asilimia 35 pekee ya Wakenya wote.
Aidha, inakadiriwa kuwa Wakenya wapatao milioni 1.5, sawa na asilimia 3 wanatumia bima ya kibinafsi kugharamia matibabu.
Huku Rais Uhuru Kenyatta akijikakamua kuimarisha huduma za afya nchini, kupitia mojawapo ya ajenda nne kuu, Afya Bora kwa Wote, upataji wa huduma bora za matibabu na kwa gharama nafuu kwa wananchi wengi ni bayana ungali kikwazo.
Waathiriwa ni wenye mapato ya chini na wafanyabiashara wadogo na wa kiwango cha kadri – SMEs, katika sekta ya Juakali.
Ili kuangazia changamoto hizo, 4G Capital Group Limited (4G Capital) ambalo ni shirika la kifedha kwa ushirikiano na kampuni ya bima ya Insurtech Innovator Turaco, imebuni mpango wa utoaji bima ya afya kwa bei nafuu. Mpango huo unalenga wafanyabiashara wa mapato ya chini na ya kadri.
4G Capital imekuwa nchini Kenya tangu 2013, ambapo imekuwa ikitoa mikopo kwa SMEs Ukanda wa Afrika Mashariki, pamoja na ushauri namna ya matumizi ya fedha na pia mafunzo jinsi ya kuimarisha biashara.
Hapa nchini, shirika hilo lina wateja 104, 000, Uganda 46, 000, na linasema kuzinduliwa kwa mpango wa bima ya afya ya bei nafuu kutasaidia kuwalinda kutokana na changamoto za kifedha zinazoibuka wanapogonjeka au kupata majeraha.
Wengi wa wateja, wanahudumu katika sekta ya Juakali na wanapougua biashara zao huwa katika hatari ya kufilisika. Kila baada ya miaka mitano hapa nchini, asilimia 42 ya wenye mapato madogo hupitia nyakati ngumu kifedha hasa wanapolazwa hospitalini kupata matibabu.
4G Capital kwa ushirikiano na Turaco, mpango wa bima iliyozindua utasaidia kupunguza gharama ya pesa inayoibuka hasa mteja anapolazwa au kufariki. Aidha, ada ya malipo ya chini katika kipindi cha miezi 12, sawa na mwaka mmoja ni Sh1, 000.
Kulingana na 4G Capital, bima hiyo italinda mteja aliyelazwa zaidi ya siku tatu hospitalini au kugharamia mazishi.
Isitoshe, kufidiwa, mteja anaweza kuwasiliana na shirika hilo kwa njia ya simu au mtandao wa WhatsApp, na kupokea fidia baada ya saa 72.
Huku janga la Covid – 19 likiendelea kuwa kikwazo kwa taifa na ulimwengu, sekta mbalimbali nchini, ikiwemo ya SMEs, zimeathirika kwa kiasi kikuu. Turaco pia inatoa huduma za bima kwa waathiriwa wa janga la corona, ambalo limekuwa kero la kimataifa. “Tunafurahia kushirikiana na Turaco kutoa huduma za bima ya afya kwa wateja wetu, hasa wakati huu wanapitia nyakati ngumu zinazotokana na athari za Covid – 19.
“Wafanyabiashara wa kiwango cha chini na cha kadri, ambao ni nguzo ya uchumi wa Kenya ndio wameathirika kwa kiasi kikuu. Kupitia ushirikiano wetu, tutaweza kuimarisha upataji wa huduma zao za matibabu,” Wayne Hennessy-Barrett, Mwanzilishi na Afisa Mkuu Mtendaji wa 4G Capital akaambia ‘Taifa Leo’ katika mahojiano ya kipekee.
Sekta ya SME inachangia asilimia 50 ya ushuru wa Kenya, huku ikiwakilisha asilimia 75 ya nguvukazi nchini.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Turaco, Ted Pantone alisema huduma za bima ya afya kwa bei nafuu kupitia ushirikiano huo, pia zinalenga kuondoa hofu inayogubika Wakenya wakati huu mgumu wa Covid – 19.
“Ingawa mambo mengi maishani hayatabiriki, upataji wa huduma bora na nafuu za afya hufai kuwa kikwazo kwa wananchi. Ni fahari yetu kushirikiana na 4G Capital kuona kuwa huduma za afya zinaimarika,” Ted akaeleza, akihimiza Wakenya kukumbatia mpango huo uliozinduliwa.
Ikizingatiwa kuwa wateja wengi wa 4G Capital ni wafanyabiashara wa mapato ya chini na ya kadri, wanaohudumu katika mazingira ya soko yanayoshuhudia misongamano ya watu, shirika hilo limeungana na wadau husika kutoa misaada ya sabuni, vitakasa mikono na vifaa vya kunawa mikono ili kuzuia kusambaa kwa Homa ya Corona.
“Lengo letu si kuimarisha uwezo wa wateja kifedha pekee, ila tunawajali. Wasimamizi, wawekezaji na wafanyakazi wetu, tumejitolea kulinda wateja wote,” anasema Wayne Hennessy-Barrett, Afisa Mkuu Mtendaji 4G Capital.
Tangu kuwepo kwa shirika hilo Afrika Mashariki, limetoa zaidi ya mikopo 900, 000 yenye thamani zaidi ya Dola 100 milioni, sawa na Sh10, 635, 000 thamani ya pesa za Kenya.
4G Capital ina jumla ya matawi 100 Kenya na Uganda, yaliyobuni nafasi za ajira kwa zaidi ya watu 500.