Siasa

Obado sasa adai chama cha ODM kimejaa udikteta

September 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEORGE ODIWUOR

GAVANA wa Migori Okoth Obado ameshutumu uongozi wa chama cha ODM kwa kukimbilia kuwarai madiwani wamwondoe mamlakani ilhali mkondo wote wa sheria kuhusu mashtaka yanayomkabili bado haujakamilika kortini.

Siku moja tu baada ya kushtakiwa kwa Bw Obado kutokana na makosa ya ubadhirifu wa fedha za kaunti, ODM iliandaa mkutano na madiwani wake jijini Nairobi ambapo iliafikiwa kwamba Bw Obado anafaa atimuliwe madarakani.

Gavana huyo sasa anasema uongozi wa ODM ni wa kidikteta na unafaa usubiri hatima ya kesi zinazomkabili kabla ya kuamua kumtimua. Alisisitiza bado hana hatia kwa kuwa kesi dhidi yake bado haijakamilika.

Kwa mujibu wa gavana huyo, mkutano huo wa Jumanne haukufaa na chama hicho kilikosea kwa kuwaita madiwani katika Jumba la Chungwa ambapo waliafikiana kumbandua uongozini.

Bw Obado hata alidai baadhi ya madiwani waliohudhuria mkutano wa ODM walilazimishwa waunge mkono uwasilishaji wa hoja ya kutokuwa na imani naye katika Bunge la Kaunti ya Migori.

Alisema madiwani hao hawakupewa muda wa kuelewa yaliyokuwa yakiendelea na kwa nini walitakiwa kuchukua hatua kumwondoa afisini.

“Madiwani wana haki ya kukumbatia mchakato wa kumwondoa Gavana afisini. Hata hivyo, inashangaza kwamba ODM inawalazimisha madiwani kuning’oa mamlakani ilhali mashtaka yanayonikabili kortini hayajaamuliwa,” akasema Bw Obado.

Akizungumza na kituo kimoja cha radio, Bw Obado ambaye anatumikia muhula wake wa pili, alisema uhusiano wake na ODM haujakuwa mzuri tangu 2013.Mnamo 2013 alishinda kiti cha Ugavana kupitia PDP baada ya kupoteza kwenye mchujo wa ODM.

Hata hivyo, alijiunga na ODM 2017 na kutetea wadhifa wake. Pia alidai kwamba ODM inapanga kumwondoa kwenye orodha ya wanachama wake kutokana na kesi ya ufisadi kortini.

“Barua nyingi zimeandikwa zikilenga kunitimua mamlakani. Chama kimekuwa kikinipiga vita tangu 2013,” akasema.

Wakati huo huo, Seneta wa Migori Ochillo Ayacko naye alimtaka Bw Obado kukoma kupigana na chama na badala yake apambane na kesi inayomkabili mahakamani.

Gavana Obado pia anakabiliwa na kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo Sharon Otieno mnamo 2018.

Vilevile anakabiliwa na wizi wa fedha za umma zinazofikia Sh73 million japo alikanusha mashtaka hayo yote.

Hapo jana, alishangaa kwa nini chama kimeamua atimuliwe ilhali Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong anayekabiliwa na mashtaka kama hayo bado yupo mamlakani.

Pia alitumia mfano wa Anne Waiguru wa Kirinyaga ambaye pia ana kesi ya ufisadi lakini hajatimuliwa na chama chake cha Jubilee.

“Chama hakijaniambia kinataka nini. Baadhi ya maafisa wake wana ajenda fiche dhidi yangu. Korti kuniambia nisiingie afisini haimaanishi kwamba mimi si Gavana,” akasema na kuongeza “Bado sina makosa hadi nipatikane na hatia.”

” Nitajiuzulu nikipatikana na makosa lakini chama hakifai kuamua mkondo unaofaa kuchukuliwa na usimamizi wa kaunti,” akaongeza.

Hata hivyo, ODM imejitetea ikisema haivumilii ufisadi na wizi wa mali ya umma.Mwenyekiti wa ODM John Mbadi pia alisema uwepo wa Naibu Gavana Nelson Mahanga kama kaimu Gavana pia hakutasaidia katika utoaji wa huduma kwa wakazi wa Migori.

“Kando na jina, Naibu Gavana hajakuwa akitekekeza majukumu yoyote. Pia hajakuwa na uhusiano wa kuridhisha na mawaziri wa kaunti,” akasema Bw Mbadi.

Kati ya madiwani wote 41, ni 37 waliohudhuria mkutano wa Jumanne na kukubali kutia saini hoja ya kumwondoa Bw Obado uongozini.

Kulingana na ODM, kubanduliwa kwa Bw Obado ni njia pekee ya kuhakikisha wakazi wa Migori wanaendelea kupokea huduma.