Waziri awasilisha ripoti ya nafasi za ajira serikalini kulingana na kabila
Na CHARLES WASONGA
KWA mara nyingine imefichuka kuwa watu kutoka kabila la Agikuyu ndio wanashikilia nyadhifa za juu katika utumishi wa umma, kulingana na ripoti iliyowasilishwa katika Seneti, Alhamisi.
Kulingana na ripoti hiyo iliyowasilishwa na Waziri wa Utumishi wa Umma Margaret Kobia, Wakikuyu wanashikilia nyadhifa 120 kati ya 416 katika serikali ya kitaifa.
Wanafuatwa na watu kutoka jamii ya Wakalenjin wanaoshikilia nafasi 45, Waluo (41), Waluhya (33), Wakamba (27), Wameru (27) na Wakisii (22).
Nao watu kutoka jamii ya Wamaasai wanashikilia nafasi 19 katika Serikali Kuu, Mijikenda (10), Taita (8), Turkana (7), Borana (7) na Embu (6).
Wengine ni Wakenya wa asili ya Kihindi (1), Gabra (3), Degodia (1), Kuria (3), Mbeere (2). Ogaden (1), Orma (2), Pokot (3), Samburu (1), Teso (4), Tharaka (1), Shirazi (1) na Tharaka (1).
Hata hivyo, Waziri Kobia alisema kulingana na matokeo ya sensa ya 2019, watu kutoka kaunti zote nchini wanawakilishwa katika safu ya juu serikalini.
“Serikali inajizatiti kutekeleza sera ya kuhakikisha uwepo wa usawa katika uajiri wa watumishi na umma na kupandishwa ngazi kwa wafanyakazi. Hii inafanywa kwa kuzingatia na kudumisha utaalamu na uhitimu ili kufikia mahitaji na ujuzi hitajika katika kazi mbalimbali za serikali,” Profesa Kobia akasema alipofika mbele ya kamati ya seneti kuhusu uwiano wa kitaifa kwa njia ya mtandao.
Akaongeza: “Nyadhifa kuu serikali pia hujazwa kupitia matangazo ambayo huchapishwa katika vyombo vya habari na usaili kuendeshwa.
Kati ya maafisa 416 wakuu serikalini, 22 ni mawaziri, 26 ni mawaziri wasaidizi, 42 ni makatibu wa Wizara, saba wako katika kundi la ajira za V, 48 wako katika kundi U na 272 wako katika kundi la ajira la T.