Siasa

Ukosefu wa fedha walemaza miradi, huduma katika kaunti

September 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KENNEDY KIMANTHI

SERIKALI zote 47 za kaunti nchini hazitaweza kugharimia miradi ya maendeleo ya kaunti au kulipia huduma za maji, matibabu, umeme na wawasilishaji wa bidhaa kwa muda wa wiki mbili zijazo baada ya kuchelewa kupokea mgao wao wa fedha kutoka kwa Hazina Kuu ya Kifedha.

Kaunti bado hazijapokea fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka huu wa kifedha, hii ikimaanisha kwamba haziwezi kutangaza utoaji tenda kwa miradi mbalimbali ya kutekelezwa kwa ajili ya raia.

Kuchelewa kupokea fedha hizo kunatokana na Bunge la Seneti kukosa kupitisha mfumo mpya wa Ugavi wa Mapato na kuchelewesha zaidi kuidhinishwa kwa Mswada wa Ugavi wa Mapato 2020.

Hali hii imesababisha kukwama kwa miradi na utoaji wa huduma kwenye sekta muhimu kama afya, maji na miradi ya ujenzi wa miundomsingi.

“Hali hii ikiendelea, kaunti hazitakuwa na pesa za kuendesha shughuli zake kuanzia Septemba 17, 2020,” akasema Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (COG), Bw Wycliffe Oparanya.

“Huduma katika kaunti zote 47 hazitakwepo na tutaamuru wafanyakazi wote waende likizo ya lazima hadi suluhu ipatikane,” akasema Gavana huyo wa Kakamega.

Taifa Leo ilibaini kwamba kaunti nyingi zimesitisha kwa muda utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku zikitatizika kulipa wafanyakazi wao mishahara.

Shughuli za kaunti zimeathirika pakubwa huku vitengo vya utoaji zabuni na uwasilishaji wa bidhaa ukiathirika pakubwa.

Kaunti nyingine nazo zinalipa mishahara lakini haziwasilishi makato ya Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF), NSSF, pensheni, mikopo na michango ya wafanyakazi kwenye vyama vyao vya ushirika.

Bw Oparanya pia alionya kwamba utata wa sasa kwenye Seneti huenda ukatoa nafasi kwa raia yeyote kufika mahakamani na kuwasilisha kesi ya kuvunjwa kwa bunge hilo kulingana na kifungu cha 258 cha katibaKaunti pia zimeshindwa kuwalipa wahudumu wa afya ambao wapo mstari wa mbele katika kutoa huduma za matibabu wakati huu wa janga la virusi vya corona.

Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria alitaja tofauti za maseneta kuhusu mbinu ya kugawa fedha kama mojawapo ya masuala yanayotishia ufanisi wa ugatuzi. ‘Karibu oparesheni zote zimesitishwa baada ya kaunti kunyimwa fedha.

Nyingi zimeathirika pakubwa kiuchumi,’ akasema Bw Wa Iria COG pia ilisema wanachama wake watafika mbele ya Kamati ya Uhasibu kwenye Seneti kupitia teknolojia ya video link hadi janga la corona litokomee hapa nchini.