Wandani wa Ruto waapa kupinga mabadiliko IEBC
Na ONYANGO K’ONYANGO
WANDANI wa Naibu Rais William Ruto sasa wanadai hatua ya serikali kukosa kujaza nafasi nne za makamishina wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni njama ya kuzima kiongozi wao kwenye kura ya 2022.
Wanadai kwamba Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga wanapanga kutumia ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) kuwateua washirika wa vyama vyao kama makamishina kisha kulemaza zaidi ushawishi wa Dkt Ruto kabla ya 2022.
Wabunge Caleb Kositany (Soy), Nelson Koech (Belgut) na Didmus Baraza (Kimilili) wamesema kuwa watapinga mabadiliko kamilifu kwenye IEBC kwa sababu makamishina watakaoteuliwa watatatiza uwaniaji wa Dkt Ruto 2022.
Nafasi nne za makamishina zilisalia wazi baada ya Naibu Mwenyekiti Connie Nkatha Maina na makamishina Paul Kurgat na Margaret Mwachanya kujiuzulu 2018.
Walimwaacha Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati na makamishina Abdi Guliye na Boya Molu pekee afisini.
Kamishina Roselyne Akombe naye alijiuzulu kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi wa marudio wa Urais mnamo Octoba 26, 2017.
Inadaiwa Rais Kenyatta na Bw Odinga wanaunga mkono pendekezo kwenye BBI kwamba makamishina wa IEBC wanafaa wateuliwe na vyama vya kisiasa.
Hata hivyo, wandani wa Dkt Ruto wanapinga hili wakiiona kama njama ya kupunguza ushawishi wake na kutatiza azma yake ya kuingia Ikulu 2022.
Bw Kositany alimtaka Rais Kenyatta ajaze nafasi ya makamishina hao haraka badala ya kubadilisha uongozi wote wa IEBC.
Mbunge huyo alishutumu ODM akisema wao ndio wanapigania sana mabadiliko IEBC kwa sababu huwa wana mazoea ya kutokubali matokeo ya uchaguzi.
“IEBC ya sasa inaweza kusimamia uchaguzi mkuu ujao. Mkumbuke kwamba ripoti ya Kriegler iliweka kifungu kilichosema kuwa huwezi kubadilisha makamishina wa IEBC, miaka miwili kabla ya uchaguzi Mkuu. Kile kinachofaa kufanyika ni kwamba makamishina wapya wanafaa wateuliwe sasa ili washirikiane na wengine kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022,” akasema.
Alisisitiza kwamba huu si wakati wa kutekeleza mabadiliko kwenye tume hiyo ila ni muda wa kuboresha utendakazi wake ili kuzuia wizi wa kura unaolalamikiwa kila mwaka wa uchaguzi.
“Mabadilko kwenye IEBC ni kinyume cha katiba na hatufai tupiganie mabadiliko yanayopendelea mrengo fulani wa kisiasa,” akaongeza.
Bw Koech naye alipinga mabadiliko kwenye IEBC akisema mrengo wa ODM unazua taharuki bure kwa kutumia njia za mkato kutafuta uongozi wa nchi.
Aliunga mkono kauli ya Bw Kositany, akihoji kwamba wabunge wa ODM walikabidhiwa uongozi wa kamati ya haki na sheria kwenye mabunge yote ili kuandaa mchakato wa kubadilisha IEBC.
“Kama taifa tutapoteza dira iwapo tutakuwa tunatekeleza mabadiliko kila mara kufurahisha ODM ambayo imekuwa ikishindwa kura kisha wanazua malalamishi,” akasema mbunge huyo wa Belgut.
Bw Barasa naye alimtaka Rais Kenyatta ateue jopo baada ya Bunge la Kitaifa na lile la Seneti kutofautiana kuhusu idadi ya watu wanaofaa kuteuliwa kupiga msasa watu wa kujaza nafasi nne za makamishina.
“Rais anafaa ateue jopo ili kutangaza siku ya mahojiano na kisha liorodheshe majina ya kuteua kwenye nyadhifa hizo za makamishina. Kuruhusu vyama vya kisiasa kuingilia suala hilo ni kosa kwa kuwa sheria inafaa ifuatwe,” akasema Bw Barasa.