• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Trump motoni kwa kuagiza wafuasi wake wapige kura mara mbili

Trump motoni kwa kuagiza wafuasi wake wapige kura mara mbili

Na AFP

RAIS wa Amerika Donald Trump amejipata matatani kutokana na matamshi yake kwamba wafuasi wake wapige kura mara mbili kwenye uchaguzi Mkuu wa Novemba 3.

Akihutubia wafuasi wake katika jimbo la Carolina Kaskazini, Rais Trump aliwataka wafuasi wake wapige kura kupitia barua pepe na wakati huo huo kufika vituoni baadaye kupiga kura kwa mara nyingine.

Alisema hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kwamba kura zao zinahesabiwa na haziibwi.

Wapigakura wengi wanatarajiwa kupiga kura kupitia barua pepe kutokana na uwepo wa virusi vya corona nchini humo.

“Nawaelekeza watume kupitia barua pepe kisha waende wapige kura vituoni. Na iwapo mfumo wa kielektroniki unaotumika utakuwa na uwazi jinsi inavyodaiwa, basi hawataweza kupiga kura mara mbili,” akasema kiongozi huyo kwenye mahojiano na runinga ya WECT akiwa jimbo la Carolina Kaskazini.

Ingawa hivyo, upigaji kura mara mbili ni kinyume cha sheria za uchaguzi na kauli ya Rais Trump inafasiriwa kwamba hana imani na mfumo wa upigaji kura nchini humo.

Baada tu ya kauli hiyo, wanaharakati walimkejeli Rais huyo na kuwataka wapigakura Marekani wampuuze. Wanaharakati hao walieleza imani yao katika utendakazi wa Tume ya uchaguzi nchini humo.

“Kupiga kura mara mbili ni haramu. Msimsikize Rais,” ukachapisha muungano wa wapiganiaji wa haki za kibinadamu nchini Marekani kwenye Twitter.

Mwanasheria Mkuu wa Marekani William Barr naye Jumatano alionekana kumuunga mkono Rais Trump, akisema upigaji kura kupitia barua pepe si salama na unaweza kuvurugwa kuwasaidia baadhi ya wawaniaji.

Alipoulizwa kuhusu matamshi yake kuwa nchi za nje zinaweza kuingilia uchaguzi huo, Barr hakufichua nchi hizo, akisema tu hilo ni suala ambalo halifai kupuuzwa.

Pia hakukemea matamshi ya Rais Trump kwamba watu wapige kura mara mbili, akitaja ulegevu wa sheria za uchaguzi wa jimbo la Carolina Kaskazini.

“Sifahamu hasa nini sheria za uchaguzi wa jimbo hilo zinasema. Huenda raia anaweza kubadilisha kura yake baada ya muda fulani. Sijui,” akasema.

Rais Trump amekuwa akishutumu Democrats kwa kupanga njama ya kuiba kura kupitia upigaji kura kwa njia ya barua pepe.

Kikosi cha kampeni cha Rais huyo tayari kimewasilisha kesi mahakamani dhidi ya Majimbo ya New Jersey na Nevada yaliyoimarisha teknolojia ya upigaji kura kupitia barua pepe.

You can share this post!

Walimu watahudumu miaka 10 kabla ya kuajiriwa – TSC

Mbunge wa Lari na maafisa wa CDF wakamatwa